Tanzania: Kamati yapendekeza kuwepo kwa ‘lockdown’ kupunguza maambukizi ya Covid-19

Tanzania: Kamati yapendekeza kuwepo kwa ‘lockdown’ kupunguza maambukizi ya Covid-19

Na LEONARD ONYANGO

WAKAZI wa maeneo yaliyo na kiwango cha juu cha maambukizi ya virusi vya corona nchini Tanzania huenda wakafungiwa ndani iwapo serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan itatekeleza kikamilifu mapendekezo ya ripoti ya kamati iliyobuniwa kutathmini ugonjwa wa Covid-19 humo nchini.

Kamati hiyo iliyoongozwa na Prof Said Aboud, inasema kuwa Tanzania tayari imekumbwa na mawimbi mawili na nchi hiyo ya Afrika Mashariki inakabiliwa na hatari ya kuyumbishwa na wimbi la tatu.

Ripoti hiyo, hata hivyo, inaonya kwamba iwapo serikali itafanya uamuzi wa kuwashurutisha watu kutoondoka nyumbani kwa lengo la kudhibiti maambukizi ya virusi vya corona, ihakikishe kwamba shughuli za kiuchumi hazitatiziki.

“Serikali iendelee kuzingatia mazingira ya Kitanzania katika udhibiti wa ugonjwa wa Covid-19 katika kuamua kuweka au kutokuweka shuruti ya kujifungia na kuwa na ubunifu ili kuruhusu ukuaji wa uchumi na kuimarisha sekta zinazochangia katika uchumi,” inasema ripoti hiyo.

Ripoti hiyo pia inaitaka serikali kutoa takwimu kuhusu uwepo wa ugonjwa wa Covid-19 na kuchukua hatua madhubuti kuimarisha hatua zote za afya za kinga katika ngazi zote ili kuepusha wimbi la tatu la ugonjwa huo.

Ripoti ya kamati hiyo pia inapendekeza kuwa serikali iagize chanjo ya corona kupitia mpango wa kutoa chanjo nafuu kwa nchi maskini (Covax).

Kuhusu tiba za kiasili, kamati hiyo inapendekeza kuwa dawa hizo zitumike lakini sharti ziwe zimethibitishwa kisayansi.

“Kamati inashauri serikali kwa kutumia vyombo vyake iendelee na hatua kuelekea kuruhusu matumizi huru ya chanjo dhidi ya ugonjwa wa Covid-19 kwa kutumia chanjo zilizoorodheshwa na Shirika la Afya Duniani (WHO) ili kuwapa fursa ya kinga wananchi wake kwa kuwa kupitia uchambuzi wa Kamati, chanjo hizo zina ufanisi na usalama unaokubalika kisayansi,” inasema ripoti hiyo.

Kamati hiyo inashauri kwamba makundi ya watu walio katika hatari kubwa ya kuambukizwa na corona yapewe kipaumbele chanjo itakapowasili nchini.

“Kipaumbele cha utoaji wa chanjo dhidi ya Covid-19 nchini kwa kuanzia kiwe kwa wahudumu katika vituo vya kutolea huduma za afya na watumishi walio katika mstari wa mbele wa utoaji wa huduma mathalani watumishi sekta ya utalii, hoteli, mipakani, viongozi wa dini na mahujaji.

“Wazee na watu wazima kuanzia umri wa miaka zaidi ya 50 na watu wazima wenye maradhi sugu mengine mathalani kisukari, shinikizo la damu, maradhi ya mfumo wa upumuaji, magonjwa ya figo pia wapewe kipaumbele,” inasema ripoti hiyo.

Iwapo, Rais Suluhu ataamua kutoa agizo la kufunga baadhi ya maeneo ya nchi, atakuwa ameenda kinyume na msimamo wa mtangulizi wake John Pombe Magufuli aliyeaga dunia Machi 17, 2021.

Magufuli alikuwa ameapa kuwa hatafunga nchi na wala hataagiza chanjo ya corona kutoka mataifa ya kigeni.

You can share this post!

Wakazi wa Nyandarua waadhimisha Siku ya Punda Nchini

TAHARIRI: Mjadala wa bangi ufanywe kimakinifu