Kimataifa

Tanzania yakataa chanjo ya kigeni, yalenga tiba ya kiasili

December 14th, 2020 2 min read

Na BERNA NAMATA

DODOMA, TANZANIA

TANZANIA haitaagiza kinga ya kuzuia maambukizi ya virusi vya corona, Wizara ya Afya imesema.

Badala yake, msemaji wa Wizara ya Afya Gerald Chami alisema, serikali inaendelea na shughuli ya kufanyia majaribio tiba za kiasili.

“Hakuna mipango ya kuagiza chanjo ya virusi vya corona kutoka ughaibuni. Wataalamu wetu wa afya na wanasayansi wanaendelea kutafiti na kufanyia majaribio matibabu ya kiasili,” akasema.

Tanzania ilipokea shehena ya dawa ya kiasili kutoka Madagascar mnamo Mei 8, mwaka huu, lakini kufikia sasa haijafichua ikiwa dawa hiyo ilisaidia wagonjwa au la.

Shirika la Afya Duniani (WHO) limeonya dhidi ya kutumia dawa za kiasili ambazo huenda zikawa hatari kwa afya.

“Tumekuwa tukiendelea vyema tangu kutokea kwa janga la virusi vya corona. Hata ikiwa chanjo hiyo ya ughaibuni italetwa humu nchini, ni sharti ifanyiwe vipimo ili kuthibitisha kwamba ni salama kwa afya,” akasema Chami.

Tanzania ilitoa msimamo huo huku wataalamu wakisema kuwa chanjo zilizotengenezwa na kampuni za Pfizer na Moderna huenda zikafika katika mataifa ya ukanda wa Afrika Mashariki mwa wa 2022. Hii ni baada ya nchi tajiri kuagiza dozi zote za chanjo hizo.

Nchi za Afrika Mashariki sasa zimeweka matumaini yake kwa mpango wa chanjo wa Gavi (Covax) unaosimamiwa na WHO.

Kuna zaidi ya chanjo 230 zinazofanyiwa majaribio kote duniani, lakini ni chanjo mbili tu ambazo zinafanyiwa majaribio barani Afrika.

Chanjo hizo zinafanyiwa majaribio nchini Kenya, Afrika Kusini na Misri.

Kenya, Rwanda na Uganda zinapanga kupata chanjo ya virusi vya corona kupitia mpango wa Covax ambao unalenga kusaidia mataifa ya mapato ya chini kupata kinga kwa gharama ya chini.

Chanjo inayotengenezwa na Chuo Kikuu cha Oxford na kampuni ya AstraZeneca ndiyo inafaa zaidi Afrika kwani inaweza kuhifadhiwa katika majokofu ambavyo tayari yanatumika barani Afrika.

Ni asilimia 20 pekee ya watu wa Afrika Mashariki wanatarajiwa kupata chanjo ya virusi vya corona kupitia mpango wa Covax.

Kulingana na Mkurugenzi wa Taasisi ya Kutafiti Idadi ya Watu Afrika, Catherine Kyobutungi, kuna uwezekano mkubwa kwamba Afrika itapata chanjo ya Covid-19 baada ya mataifa tajiri duniani kupatia raia wao.

“Afrika huenda ikapata chanjo ya virusi vya corona kufikia mwishoni mwa 2022,” akasema Kyobutungi.

Mataifa yatakayonufaika na chanjo kupitia mpango wa Covax yatahitajika kulipia chanjo hiyo kati ya Sh160 na Sh200 kwa kila dozi.

Wizara ya Afya ya Uganda ilisema Jumatatu kuwa imeagiza chanjo hiyo kupitia mpango wa Covax.

“Hatutaagiza chanjo hiyo moja kwa moja kwa sababu ni ghali mno,” akasema Emmanuel Ainebyoona, msemaji wa Wizara ya Afya.