Kimataifa

Tanzania yapata treni za umeme, Kenya ikisukuma maisha na za kizamani

February 29th, 2024 3 min read

MWANANCHI Na CHARLES WASONGA

SHUGHULI za uchukuzi kwa treni za kutumia umeme zikitarajiwa kuanza rasmi nchini Tanzania kuanzia Julai 2024, Kenya inaendelea kutumia treni za kutumia kawi ya mafuta katika reli ya kisasa (SGR).

Jaribio la kwanza la treni ya umeme ikiwa na mabehewa manne liliendeshwa Jumatatu katika ruti ya kutoka Dar es Salaam kuenda Morogoro.

Safari hiyo ilichukua muda wa saa mbili na dakika 20 pekee.

Basi la abiria hutumia saa nne kutoka Dar es Salam hadi Morogoro.

Treni hiyo ilifanya safari ya kurudi kutoka Dar hadi Morogoro kwa kutumia saa mbili na dakika 19.

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania (TRC) Masanja Kadogosa alisema kuwa treni hiyo ya umeme ilienda kwa kasi ya kilomita 100 hadi 120 kwa saa kwa sababu katika majaribio, umakini ulihitajika pakubwa.

“Ingawa makadirio ya wastani ya kasi huwa kilomita 160 kwa saa, vichwa vyetu vinaweza kuenda hadi spidi ya kilomita 200 kwa saa. Hii ni licha ya kwamba kwenye kona huwezi kuenda kwa spidi hiyo, ni kinyume na masharti tuliyopewa,” akasema Kadogosa.

Hata hivyo, kutoka kitua cha SGR cha Posta hadi Pugu, kwa mujibu wa Kadogosa, treni hiyo iliende kwa kasi ya kilomita 50 kwa saa kutokana na ujenzi unaoendelea.

Afisa huyo alisema safari rasmi za treni za umeme zitaanza mwishoni mwa Julai 2024, kutokana na agizo la Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan.

Treni hiyo iliyofanyiwa majaribio itafanya safari  kutoka Dar es Salaam hadi Dodoma, baada ya kuunganisha kipande cha Dodoma.

Kuhusu nauli, Kadogosa alisema wameshawasilisha mapendekezo kwa Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri Ardhini (Latra), lakini kutokana na ubora wa huduma itaongezeka kidogo kulinganisha na ile ya basi.

Swali la wengi lilikuwa umeme ukikatika katikati ya safari nini kinaweza kutokea.

Kadogosa alisema kwa sasa hawatumii umeme mwingi.

“Kama tutaanza ile ya safari ya Mwanza hadi Kigoma hapo ndipo tutahitaji umeme mwingi, ingawa tuna ‘transimition line’ ambayo inajitegemea inahusu reli tu sio kitu chochote,” akasema.

Alisema hata ikitokea nchi nzima hakuna umeme, treni itaendelea kufanya kazi.

“Kuna vichwa vinatumia umeme na dizeli, ikitokea umeme umekatika, abiria hawezi kujua… tuna-switch tu, hiyo ni kwa ajili ya tahadhari kama itatokea nchi nzima haina umeme. Kwa sasa Dar es Salaam ukikatika, sehemu nyingine utakuwepo,” akaeleza.

Ikiwa na mabehewa manne, mawili ya business (daraja la juu) na mengine economy (daraja la kati), treni hiyo ilianza safari saa nne na nusu asubuhi kwenye stesheni ya SGR Dar es Salaam na kuwasili Morogoro saa saba kasoro dakika 10 mchana.

Njiani, ikiwa imetembea kwa dakika 30, umeme wa ndani ya treni ulikatika kwa baadhi ya taa, soketi za kuchaji simu na viyoyozi kuzima, lakini treni iliendelea na safari bila abiria kuhisi chochote.

Muda mfupi badaye ulirejea na kukatika tena saa 5:18 na saa 5:59 lakini mara zote ulirejea baada ya mfupi, huku mara zote treni ikiendelea na safari, japo kila umeme ulipokatika kuna nyakati lilipunguza mwendo.

Masha Yassin, Ofisa Usafirisha Mwandamizi wa TRC amesema kuna vituo ilikuwa ikifika inabidi kuingiza umeme wa phase nyingine.

“Hiyo inaitwa nutro zone, maana kuna phase one, two na kuendelea, hivyo ili umeme wa phase nyingine uingie lazima wa phase nyingine ukate, ndicho kilikuwa kinatokea umeme unakata na kurudi ndani ya muda mfupi,” alisema.

Akizungumzia safari ya Jumatatu ya majaribio, Kadogosa alusema ni ya tofauti, kwani ilikuwa na mabehewa.

“Mwanzo tulikuwa tunafanya majaribio ya kichwa cha treni hii tu, leo (mnamo Jumatatu) tumefunga mabehewa manne, ingawa inaweza fungwa mabehewa 12 hadi 15,” akasema.

Kutoka Stesheni Dar es Salaam, treni hiyo ilianza safari kwa mwendo wa kawaida, huku baadhi ya wakazi wa Jiji la Dar es Salaam wakiacha shughuli zao na kuifurahia, wengine wakiipungia mikono na wengine kuchukua video na picha mnato kwa simu.

Ndani ya mabehewa, kwenye daraja la ‘Economy’ mabehewa yake yana vitu vya 3 by 3 (siti za watu watatu watatu) na nyingine za 2 by 2 (wawili wawili), yakiwa na meza ndogo ya chakula kwenye kila kiti na kabati ndogo ya ukutani ya kutundika suti au nguo za aina hiyo.

Unaweza kuhama kutoka behewa moja kwenda jingine, ingawa pia huwezi kufanya hivyo kama mlango wa behewa lako umefungwa, hadi ufunguliwe na mhudumu.

Pia huruhusiwi kuweka mizigo chini ya kiti, kuna eneo maalumu la kuweka mizigo. Mradi wa treni ya umeme nchini ulianza mwaka 2017 na kuzinduliwa na Rais wa awamu ya tano, hayati John  Magufuli na kuendelezwa na mrithi wake, Suluhu Hassan.

Awamu ya kwanza kati ya Dar es Salaam mpaka Morogoro ulielezwa ungekamilika ndani ya miezi 30 mpaka kufikia Novemba 2019, jambo ambalo halikuwezekana.

Iliongezwa miezi 18 mpaka Aprili, 2021, ikashindikana pia.

Aliyekuwa Waziri wa Ujenzi wakati huo, Leonard Chamuriho akaeleza reli hiyo ingeanza kufanya kazi ndani ya miezi minne, yaani Agosti 2021, ikashindikana tena.

Januari 17, 2022, aliyekuwa Msemaji Mkuu wa Serikali wakati huo, Gerson Msigwa alieleza kuwa awamu ya kwanza ya kipande cha Dar es Salaam mpaka Morogoro ungekamilika na majaribio yangeanza Aprili 2022, haikuwezekana hadi jana majaribio ya kwanza yalipoanza.

Msemaji Mkuu wa Serikali, Mobhare Matinyi aliyekuwa sehemu ya safari hiyo amesema majaribio hayo ni uthibitisho wa Serikali kutimiza ahadi zake ikiwemo ile iliyotolewa na Rais mwishoni mwa mwaka 2023 na kwamba mpaka Julai 2024 treni hiyo itaanza safari zake.

“Tuna miezi michache kufika Julai na tayari tumefanya majaribio ya kwanza na tunatarajia kufanya majaribio mengine kutoka Dar es Salaam mpaka Dodoma na kurudi na hatimaye zitakuja kuanza shughuli rasmi za kibiashara treni zikibeba abiria na mizigo,” alisema Matinyi.

Awali, ahadi ya kuanza kwa safari hiyo ilitolewa na Kadogosa akisema zingeanza Desemba 2022.