Habari za Kitaifa

Tanzania yapiga marufuku ndege za Kenya Airways katika hatua ya kulipiza kisasi

January 15th, 2024 2 min read

UPDATE: Tanzania, Jumanne Januari 16, 2024 imeondoa marufuku hiyo baada ya makubaliano ya Kenya kuruhusu ndege za uchukuzi wa mizigo kuhudumu nchini Kenya. Habari kamili inafuata – Mhariri

NA WANDERI KAMAU

TANZANIA imesimamisha safari zote za ndege kutoka Nairobi hadi Dar es Salaam kuanzia Januari 22, 2024.

Kwenye taarifa Jumatatu, Mkurugenzi Mkuu wa Halmashauri ya Kusimamia Safari za Ndege ya Tanzania (TCAA), Hamza Johari, alisema kuwa hilo linafuatia hatua ya Kenya kukataa ndege za kubeba mizigo kutoka shirika la ndege la Tanzania—Air Tanzania— kusafiri nchini.

“Hili ni jibu kwa Kenya kufuatia hatua yake kukataa ombi la shughuli zote za ndege za kubebea mizigo kutoka Air Tanzania, kati ya Nairobi na Dar es Salaam. Hili ni kinyume na Mwafaka wa Makubaliano kuhusu huduma za ndege baina ya Kenya na Tanzania uliotiwa saini  Novemba 24, 2016, jijini Nairobi,” akasema Johari.

Akaongeza: “Jamhuri ya Tanzania itakuwa ikijaribu kila mara kuzingatia kanuni za Mkataba wa Chicago kuhusu Huduma za Ndege baina ya mataifa jirani.”

Hatua hiyo inaonekana kufufua tofauti za kimahusiano ambazo zimekuwepo baina ya Kenya na Tanzania kwa muda mrefu.

Uhusiano wa mataifa hayo mawili ulidorora sana wakati wa uongozi wa Rais Mstaafu Uhuru Kenyatta na aliyekuwa rais wa Tanzania, marehemu John Magufuli.

Hata hivyo, Rais Samia Suluhu Hassan amekuwa akijaribu kuboresha uhusiano wa Tanzania na Kenya baada ya kuchukua uongozi mnamo 2020, kufuatia kifo cha Dkt Magufuli.

Ikizungumza kuhusu tukio hilo, usimamizi wa Kenya Airways umesema kwamba umeanza majadiliano na Halmashauri ya Kusimamia Safari za Ndege za Tanzania (TCAA) kuona kwamba huduma hazitatatizwa.

“Kenya Airways (KQ) imepata taarifa kwamba TCAA imesitisha ruhusa kwa KQ kufanya safari za abiria kati ya Nairobi na Dar es Salaam kuanzia Januari 22, 2024. Tunashauriana na utawala nchini Tanzania na mashirika mengine ya kiserikali baina na nchi hizi mbili kuona kwamba tunapata suluhu ambayo itahakikisha kwamba huduma za ndege hazitakatizwa kati ya Nairobi na Dar es Salaam,” ikasema taarifa ya KQ.

Wadau na umma kwa jumla utakuwa unafuatilia kuona jinsi mgogoro huo utatatuliwa haraka iwezekanavyo.