Habari

TANZIA: Askofu Mstaafu Ndingi Mwana'a Nzeki afariki

March 31st, 2020 1 min read

NA FAUSTINE NGILA

Askofu Mkuu Mstaafu wa Kanisa Katoliki Ndingi Mwana a’ Nzeki amefariki jijini Nairobi Jumanne asubuhi akiwa na miaka 89.

Askofu Mkuu wa kanisa hilo humu nchini John Njue alitangaza kifo cha Mwana a’ Nzeki  kupitia kwa ujumbe ulioandikwa na Padri John Njau na kutumwa kwa vyombo vya habari.

“Ni asubuhi ya majonzi  baada ya John Cardinal Njue kutangaza kifo cha Askofu Emeritus Raphael Ndingi Mwana ‘a Nzeki,” Dayosisi ya Kanisa Katoliki ya Nairobi  ilitangaza kwenye mtandao wa kijamii wa Facebook.

“Natuombe mungu ailaze roho yake pema peponi,” ulisema ujumbe huo.

Mwana a’Nzeki alizaliwa Desemba 25, 1930 katika Kaunti ya Machakos na alikwezwa kuwa askofu na Papa Paul VI.

Alihudumu katika dayosisi ya Machakos kutoka 1969 hadi 1971 na Nakuru kutoka 1972 hadi 1996.

Mnamo mwaka 1997, alichukua hatamu za uongozi wa dayosisi ya Nairobi hadi alipostaafu mwaka wa 2007.

Askofu huyo amekuwa akiugua kwa muda mrefu.