Bambika

Tanzia: Ex-mume wa Lady JayDee aaga dunia

April 20th, 2024 2 min read

NA SINDA MATIKO

ALIYEKUWA mumewe nyota mkongwe wa Bongo Flava Lady JayDee, mtangazaji maarufu Gardner ‘Captain’ Habash amefariki dunia.

Habash ambaye hadi kifo chake alikuwa ni mtangazaji wa Clouds FM, alifariki dunia mapema Jumamosi akiwa na umri wa miaka 51.

Mtangazaji huyo mkongwe aliyejizolea umaarufu mkubwa kutokana na utangazaji wake lakini pia kupenda kuibua skendo mara kwa mara, alikuwa akitatizwa na ugonjwa wa shinikizo la moyo.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na uongozi wa Kampuni ya Clouds Media Group, inayoimiliki Clouds FM, Gardner alimaliza mwendo duniani wakati akiwa anaendelea kupata matibabu katika hospitali taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), iliyoko jijini Dar es Salaam alikokuwa amelezwa kwa siku kadhaa.

Taarifa hiyo imeeleza kwamba Captain alikuwa akitatizwa na tatizo la shinikizo la damu, kabla ya mauti kumkuta na afya yake ilikuwa tayari imedorora.

“Clouds Media inasikitika kutoa taarifa ya kifo cha Gardener G Habash ambaye alikuwa mtangazaji wa kipindi cha Jahazi kilichotokea usiku wa kuamkia leo. Tunatoa pole kwa ndugu, jamaa, marafiki, wafanyikazi wenzake na mashabiki wa Captain G Habash,” taarifa ya Clouds Media ilisema.

Hadi kifo chake, mtangazaji huyo mkongwe alikuwa ameitumikia Clouds FM kwa zaidi ya miaka 20, huku akiendesha kipindi cha Jahazi hadi 2010 alipotangaza kuchukua mapumziko madogo.

Gardner alirejea tena Clouds Aprili 2016 na kuendelea kuitumikia stesheni hiyo hadi mauti yalipomfika.

Licha ya kuwa na taaluma ya kufana kwenye utangazaji na kuweza kujitengenezea jina na sifa kubwa miongoni mwa watangazaji bora kuwahi kutokea Tanzania, ustaa na umaarufu wa Captain uliongezeka maradufu hasa katika miaka ya awali ya 2000s alipoanzisha mahusiano ya kimapenzi na staa Jide.

Baada ya kudeti kwa miaka minne, kapo hiyo ya mastaa wakubwa wa showbiz Tanzania enzi hizo, ilifunga ndoa 2005.

Hata hivyo ndoa yao ilidumu kwa miaka tisa tu ikivunjika 2015 mwaka ambao iliingiwa na mdudu na kuwapelekea wawili hao kutengana.

2016, Jide aliamuwa kuwasilisha rasmi maombi ya talaka mahakamani, utaratibu ambao ulikamilishwa rasmi 2020.

Mahusiano ya Jide na Gardner yaliangaziwa pakubwa sana kipindi mapenzi yakiwa yameshamiri lakini hata pale ndoa ilikumbwa na misukosuko.

Kuelekea wawili hao kuachana, waliishia kugeukiana na kuwa maadui wakubwa.

Kwenye mojawapo ya mahojiano aliyoyafanya 2016, Jide alidai sababu za kuamua kumtaliki Gardner zilichochewa na tabia zake za kumchepukia mara kwa mara lakini pia, uraibu wake wa kupenda pombe.

Hata hivyo miaka michache baadaye wawili hao walizika tofauti zao na kuanza kuonekana viwanjani pamoja na kukazuka uvumi kwamba wamerudiana.

Lakini Jide alipinga ripoti hizo akisisitiza kuwa hawawezi kurejesha penzi baina yao na kwamba walikuwa wamemaliza tofauti zao na kusalia marafiki tu.

Gardner amemwacha mtoto mmoja mwanamuziki Malkia Karen ambaye alimpata kutoka mahusiano mengine.

Gardner na Jide hawakuwahi kufanikiwa kupata mtoto.