TANZIA: Hillary Ng’weno afariki, aacha historia ya kutamaniwa na wanahabari

TANZIA: Hillary Ng’weno afariki, aacha historia ya kutamaniwa na wanahabari

Na CHARLES WASONGA

KWA mara nyingine taaluma ya uanahabari imepata pigo kufuatia kifo cha mwanahabari mwingine mkongwe.

Hillary Boniface Ng’weno, ambaye anafahamika kama mwasisi wa lililokuwa jarida la kila wiki “Weekly Review”, alijijengea himaya ya sifa miaka ya ‘80s na ’90s kutokana na weledi wake katika uchambuzi wa masuala ya kisiasa nchini Kenya.

Ng’weno, 83, alifariki Jumatano baada ya kuugua kwa kipindi cha miaka mitatu.

Kulingana na wanawe wa kike, Amolo Ng’weno na Bettina Ng’weno, baba yao alianza kuugua baada ya kusherehekea miaka 80 tangu kuzaliwa kwake.

“Tangu wakati huo, afya yake imeendelea kudhoofika na hatimaye alifariki leo, siku 10 tu baada ya kuadhimisha miaka 83 baada ya kuzaliwa kwake,” wakasema kwenye taarifa Jumatano.

“Alifariki nyumbani akitunzwa na familia yake,” Amolo na Bettina wakaongeza.

Ng’weno ambaye ana tajriba ya miaka 40 katika uanahabari alizaliwa jijini Nairobi mnamo mwaka wa 1938. Aliasisi jarida la Weekly Review mnamo 1975 jarida ambalo pia lilichambua masuala ya kiuchumi.

Japo alisomea somo la Fizikia katika Chuo Kikuu cha Harvard, Amerika, alibadili taaluma na kukumbatia uanahabari. Hapo ndipo akaajiriwa kama ripota wa magazeti ya Daily Nation. Alipanda cheo na mnamo 1965, akiwa na umri wa miaka 26 pekee Ng’weno aliteuliwa kuwa Mhariri Mkuu wa kwanza Mwafrika wa “Daily Nation”.

Hata hivyo, alijiuzulu wadhifa huo baada ya kuhudumu kipindi cha miaka michache baada ya kutofautiana na wamiliki wa gazeti hilo, waliosisitiza kuwa “Mzungu wa asili ya Uingereza awe nyapara wa Ng’weno.”

Hata hivyo, Ng’weno aliendelea kuandika makala ya kuvutia ya ucheshi, hususan kuhusu mada za kisiasa.

Mwendazake, ambaye alijulikana na wanahabari wenzake kwa jina Hilary au kwa herufi za jina lake kamili, HBN, pia alifanya mengi katika kitengo cha utangazaji na utayarishaji wa vipindi vya televisheni.

Mnamo 1986 alitayarisha kipindi cha drama kwenye runinga, kwa jina “Usiniharakishe” . Kipindi hiki ambacho kilipeperushwa katika runinga ya shirika la habari nchini, KBC kilibeba maudhui ya ngono miongoni mwa vijana. Hii ndio maana kipindi hicho kilipigwa marufuku baada ya maonyesho mawili pekee.

Baadaye katika miaka ya 1980s, Ng’weno alianzisha kituo cha kwanza cha kibinafsi nchini kwa jina, STV. Baadaye kituo hicho cha runinga kilinunuliwa na kampuni ya Mediamax, kinachohusishwa na Rais Uhuru Kenyatta.

Japo jarid la “Weekly Review’ lilisambaratika mnamo mwaka wa 2001, Ng’weno aliendelea kuandika makala na kutayarisha vipindi yenye maudhui ya kisiasa kwa ushirikiano na Shirika la Habari la Nation Media Group (NMG). Aliandaa vipindi kuhusu siasa za Kenya, vilivyoshinda tuzo. Vipindi hivyo vilijulikana kama “Makers Of Nation”.

Hilary Ng’weno ameacha mjane, Fleur Ng’weno, na mabinti zake wawili; Amolo Ng’weno Dkt Bettina Ng’weno.

You can share this post!

Aliyekuwa mchezaji wa Harambee Stars aendelea kutatizika...

Jamii ndogo zataka Rais abuni wizara iwasaidie