TANZIA: Huzuni baada ya mchezaji nyota wa Tong-IL Moo-Do kufariki

TANZIA: Huzuni baada ya mchezaji nyota wa Tong-IL Moo-Do kufariki

NA ABDULRAHMAN SHERIFF

RAIS wa Shirikisho la Tong-IL Moo-Do la Kenya, Clarence Mwakio amesema kifo cha Gordon Ochieng (pichani) kimewahuzunisha maafisa wa shirikisho, wachezaji wenzake wa spoti hiyo na washikadau kwani alikuwa akipigania taifa lake nyakati za mashindano ya kimataifa.

Mchezaji huyo wa Tong-IL Moo-Do Gordon Ochieng aliaga dunia kufuatia ajali ya barabarani Jumatatu huko Bondo, Kaunti ya Siaya.

“Ni kwa masikitiko makubwa kutangaza kifo cha Gordon Ochieng, mshindi wa medali ya dhahabu katika Mashindano ya Dunia ya Chungju World Martial Arts Masterships Korea na aliyefanikiwa kushinda medali kadhaa za mashindano ya Mombasa Open. Tumewasiliana na familia yake kufuatia kifo chake cha ghafla kilichotokana na ajali iliyotokea Bondo. Tuiweke familia katika maombi katika kipindi hiki kigumu, tukisubiri mawasiliano zaidi,” ikasema taarifa hiyo.

Mwakio ambaye pia ni rais wa Shirikisho la Tong-IL Moo-Do amesema wamempoteza mchezaji wa timu ya taifa ya Jasiri ambaye katika kila mashindano ya kimataifa, alikuwa akipigania ushindi kwa ajili ya kuipatia sifa nchi yake.

Kwa niaba ya wachezaji wenzake wa Jasiri, nahodha Elvis Malipe amesema wako pamoja na familia ya marehemu katika kuomboleza kifo cha mwenzao ambaye alikuwa mchezaji aliyependa kushirikiana na wenzake na kutaka maoni ya jinsi ataweza kuishindia nchi yake medali.

“Nimekuwa na Ochieng wakati anapowakilisha taifa lake alikuwa nah amu ya kuhakikisha haondoki mashindanoni bila ya kuipatia kenya medali kadhaa zikiwemo za dhahabu, fedha na shaba,” akasema Malipe aliyesema wamempoteza mchezaji aliyekuwa miongoni mwa wale bora.

Katika mashindano ya 2019 Chungju World Martial Arts Masterships, Ochieng aliyekuwa na umri wa miaka 29 alishinda medali ya dhahabu katika kitengo cha Heavyweight Free Sparring na akashinda medali mbili za fedha kwenye mashindano ya Mombasa Open vitengo vya uzani mkubwa vya Free Sparring na Special Techniques.

  • Tags

You can share this post!

PAC yatisha kukatiza pesa za mashirika, wizara ambazo wakuu...

Ubelgiji yapata kocha mpya

T L