Makala

Tanzia katika Fasihi: Kauli za wanafalsafa

April 19th, 2019 3 min read

Na WANDERI KAMAU

MABADILIKO mengi yameipitikia dhana ya tanzia tangu ilipozungumziwa na Mwanafalsafa Aristotle.

Jambo muhimu analosisitiza mwanafalsafa huyo ni kwamba: “Hakuna anayeweza kupangua lililopangwa.”

Vilevile, Aristotle anatilia mkazo matokeo ya tanzia; yaani hofu na huruma.

Katika miaka iliyofuatia, dhana hii ilibadilika.

William Shakespeare katika tanzia zake anampa mhusika-tanzia uhuru wa kujichagulia msimano anaotaka kuufuata.

Uchaguzi huu ndio unaomsababishia mhusika huyo fanaka au taabu.

Hali hizi zinatokea katika tamthilia za ‘Makbeth’ na ‘Juliasi Kaizari’. Naye mwanafalsafa Hegel (1971), anaiona tanzia katika muktadha wa makali ya migogoro inayosababisha mgawanyiko wa nafsi ya mhusika.

Kwa mujibu wa Hegel, jaribio la kusuluhisha migogoro migumu ya kinafsia ndicho kiini cha tanzia.

Hegel aliisoma upya tamthilia ‘Antigone’ iliyotungwa na Sofokile akitumia nadharia yake ya upembuzi.

Kutokana na uhakiki wa Hegel, mgogoro kama sifa isiyoweza kutengeka na tamthilia uliimarishwa ukawa nguzo muhimu ya tamthilia popote ilipoandikwa.

Katika miaka iliyofuatia, Vita vya Dunia vya Kwanza na vya Pili, tanzia ilihusishwa na sanaa tendaji inayodunisha au ubwege.

Wahusika ambao walitawaliwa na ulimwengu uliokinai maadili ya kidini na mantiki ya kisayansi walikuwa wahusika tanzia. Hawa wahusika wanapatikana katika tamthilia za Samuel Beckett.

Katika fasihi ya Kiswahili, ubwege umehusishwa na tamthilia ‘Amezidi’ (1995) yake Said Ahmed Mohamed.

Hivi sasa katika nyakati zetu, baadhi ya watunzi na wahakiki wanazungumzia tanzia yenye kusawiri matumaini. Tanzia hizi huhubiri matumaini licha ya misiba inayowakuta wahusika wakuu.

Katika fasihi ya Kiswahili, wahusika hawa ni kama vile: Kinjeketile, Mzalendo Kimathi na Mukwava.

Fikra za Aristotle kuhusu Utendi

Pamoja na kuzungumzia tanzia, Aristotle anajadili juu ya utendi. Anasema kuwa utendi unafanana na tanzia katika sifa zifuatazo:

(i) Kwa upande wa kuzungumzia kadhia moja kuu inayojitosheleza.

(ii) Utendi unaweza kuwa rahisi au mgumu.

(iii) Utendi una mawazo, sehemu ya kati na mwisho.

Nazo tofauti zilizoko kati ya utendi na tanzia ni: utendi ni mrefu zaidi na kinyume na tanzia hutumia arudhi.

Pili, mtunzi ana uhuru na fursa ya kuigiza visa vingi vinavyostaajabisha katika utendi kwa sababu baadhi ya matukio yanayotendeka ni ya kimiujiza.

Tanzia mara nyingi huumbwa kutokana na kadhia zinazoweza kutendeka.

Kwa ujumla, maoni ya Aristotle ni muhimu sana katika kuelewa fasihi.

Jambo analolimulikia mwanga Aristotle ni umuhimu wa ploti katika uundaji wa kazi ya Sanaa.

Ploti au msuko ni jinsi hadithi inavyoendelezwa hadi matukio ya mwisho yanapotokea. Wahusika nao ni viumbe wanaotumiwa na mwanasanaa kukuza vitushi vya maigizo yake.

Kwa jumla, fikra za Aristotle zinazorutubisha weledi wa fasihi ni hizi:

(i) Anasema kwamba fasihi si uigo wa kikasuku. Ni ubunifu unaomwezesha binadamu kumkaribia Mungu.

(ii) Ploti au msuko ni muhimu sana katika ubunifu wa Sanaa.

Jambo hili linaonyeshwa pale ambapo Aristotle anazungumzia tanzia na utendi.

(iii) Aristotle anatuonyesha kwamba fasihi itaeleweka vizuri zaidi ikiwa itagawanywa katika tanzu tofauti tofauti.

(iv) Aristotle anasema kwamba fasihi inajitosheleza na inajitawala. Haina haja kutemea taaluma nyingineyo. Haya ni kinyume na Plato, ambaye aliitazama fasihi katika muktadha wa Jamhuri Dhahania.

Horace

Alikuwa Mroma. Alizaliwa mwaka wa 65BBK.

Horace aliyachukua mawazo ya Aristotle na kuyageuza kuwa sheria zilizopaswa kufuatwa na watunzi chipukizi.

Katika makala yake, The Art of Poetry ambayo yamenukuliwa na S.T Dorsch katika makala yake katika kitabu chake, Classical Literary Criticism, Horace anaorodhesha baadhi ya haya maelekezo:

(i) Fasihi lazima ilenge kuadili na kusisimua

(ii) Tamthilia lazima iwe na maonyesho matano

(iii) Utungaji mzuri unatokana na uigaji wa kizazi cha watunzi mashuhuri walioishi zamani za kale.

Longino

Huyu alikuwa Mgiriki aliyeishi mnamo Karne ya Tatu BBK.

Katika ithibati za fasihi ya Kimagharibi, alikuwa mtaalamu wa kwanza kuzungumzia fasihi kwa kuzingatia athari zake za kisaikolojia.

Kulingana na maoni ya Longino, ubora wa kazi ya fasihi unatokana na jinsi kazi hiyo inavyoathiri moyo wa msomaji.

Katika makala ijayo, tutaangazia mihimili aliyoamini kama nyenzo kuu za fasihi.

[email protected]