Habari za Kitaifa

Tanzia: Kimunya aomboleza kifo cha mkewe

January 30th, 2024 1 min read

NA WANDERI KAMAU

MKEWE aliyekuwa mbunge wa Kipipiri Amos Kimunya, Bi Lucy Kimunya ameaga dunia Jumanne, alipokuwa akipokea matibabu katika Nairobi Hospital.

Bi Kimunya alifariki Jumanne asubuhi, kulingana na taarifa iliyotolewa na kiongozi huyo kupitia ukurasa wa akaunti yake ya X (zamani Twitter).

Bw Kimunya alihudumu kama Kiongozi wa Wengi katika Bunge la 12 na Waziri katika serikali ya Rais Mstaafu (marehemu) Mwai Kibaki.

Kwenye taarifa, Bw Kimunya alisema kuwa mkewe alifariki alipokuwa akipokea matibabu katika Nairobi Hospital.

“Ni kwa masikitiko makubwa natangaza kuwa mke wangu alifariki Jumanne, saa tisa alfajiri, alipokuwa akipokea matibabu katika Nairobi Hospital,” akasema.

Akimwomboleza mkewe, Bw Kimunya alisema marehemu alikuwa nguzo kuu katika maisha yake ya kibinafsi na kisiasa.

Akisifia vitendo vyake vizuri, mbunge huyo wa zamani alisema mkewe alitoa mchango mkubwa kuisaidia jamii kupitia mipango mbalimbali.

Alisema marehemu alikuwa akiwasaidia sana wanawake na vijana.

“Nenda vyema, mpendwa wetu Lucy, tutakukosa sana. Tutatoa taarifa zaidi,” akasema.

Bw Kimunya alihudumu chini ya marais wawili; Bw Kibaki na Rais Mstaafu Uhuru Kenyatta.

Alishikilia nyadhifa tofauti kwenye Bunge la Kitaifa na katika Baraza la Mawaziri.

Mnamo 2002, aliteuliwa na Bw Kibaki kama Waziri wa Ardhi. Mnamo 2006, aliteuliwa Waziri wa Fedha baada ya mtangulizi wake, David Mwiraria, kujiuzulu.

Bw Kimunya alijiuzulu kama Waziri mnamo Julai 2008, lakini akateuliwa tena na Bw Kibaki kama Waziri wa Bishara miezi mitano baadaye.

Alitwaa ubunge tena mnamo 2017 chini ya chama cha Jubilee. Mnamo 2019, Bw Kimunya aliteuliwa kuwa Kiongozi wa Wengi katika Bunge la Kitaifa, na kuchukua nafasi ya Aden Duale (aliyekuwa mbunge wa Garissa Mjini).

Alishindwa na Bi Wanjiku Muhia wa chama cha UDA kwenye uchaguzi wa Agosti 9, 2022.

Baadhi ya viongozi ambao wamemtumia rambirambi ni Katibu Mkuu wa chama cha Jubilee, Jeremiah Kioni.