Habari Mseto

Tanzia mamake Askofu JJ Gitahi akiaga

March 17th, 2024 1 min read

NA WANDERI KAMAU

MAMAKE mhubiri maarufu katika eneo la Mlima Kenya, Askofu JJ Gitahi, Bi Dorcas Gitahi, ameaga dunia.

Bi Gitahi aliaga dunia Jumapili, Machi 17, 2024 mwendo wa saa tano asubuhi, kulingana na taarifa iliyotolewa na askofu huyo.

Bi Gitahi amekuwa akiugua kwa muda mrefu, na alikuwa amelazwa katika Hospitali ya Mafunzo na Rufaa ya Chuo Kikuu cha Kenyatta, Kaunti ya Kiambu, alikokuwa akipokea matibabu.

“Kwa marafiki wangu, ndugu na dada, ni kwa masikitiko makubwa ninawatangazia kifo cha mamangu mpendwa, Dorcas. Mamangu alituacha mwendo wa saa 5.22 asubuhi, alipokuwa akipokea matibabu katika Hospitali ya Mafunzo na Rufaa ya Chuo Kikuu cha Kenyatta. Ahsanteni nyote kwa upendo na usaidizi ambao mmempa kwa wakati huu wote,” akasema Askofu JJ, kupitia taarifa.

Askofu huyo ni miongoni mwa wahubiri ambao wamejijengea jina katika eneo la Mlima Kenya kupitia vipindi vya mahubiri kwenye vituo tofauti vya redio na televisheni kwa zaidi ya miaka 20.

Yeye ndiye mwanzilishi na kiongozi wa kanisa la Priesthood, lililo katika eneo la Kahawa Sukari, Kaunti ya Kiambu.

Kufuatia hilo, ‘macelebs’ maarufu kutoka ukanda huo—wakijumuisha wanamuziki, watangazaji na wahubiri wenzake—waliungana kumtumia jumbe za pole wakati huu mgumu wa maombolezo.

Baadhi ya watu waliotuma jumbe hizo ni mwanamuziki Karangu Muraya, Muigai wa Njoroge, Betty Bayo kati ya wengine wengi.

“Ninaungana na ndugu yangu, Askofu JJ kumwomboleza mamake, Bi Dorcas. Si jambo rahisi kumpoteza mzazi. Nakuombea nguvu na uvumilivu wakati huu mgumu,” akasem Bw Muraya.

Maelfu ya mashabiki wa mhubiri huyo pia walimtumia jumbe za rambirambi.