TANZIA: Mbunge wa Juja afariki

TANZIA: Mbunge wa Juja afariki

SIMON CIURI na CHARLES WASONGA

MBUNGE wa Juja Francis Munyua Waititu amefariki baada ya kuugua kansa ya ubongo kwa kipindi kirefu.

Kulingana na familia yake, Bw Waititu, 62, alifariki Jumatatu saa moja na nusu usiku katika Hospitali ya MP Shah Nairobi ambako alikuwa akitibiwa.

“Alifariki katika hospitali ya MP Shah ambako alikuwa amelazwa tangu Februari 12, 2021, baada ya hali yake kuwa mbaya. Amekuwa akiugua kansa kwa muda mrefu na amewahi kupelekwa India kwa matibabu zaidi,” Michael Waititu, ambaye ni mwanawe mbunge huyo, akaambia Taifa Leo kwa njia ya simu.

“Mwili wake umepelekwa katika hifadhi ya maiti ya Lee, Nairobi na mipango ya mazishi itaanza katika makazi yetu jijini Nairobi na Juja,” akaongeza.

Marehemu Waititu, almaarufu ‘Wakapee’ alipatikana na ugonjwa wa saratani mnamo mwaka wa 2017.

Rais Uhuru Kenyatta na Spika wa Bunge la Kitaifa Justin Muturi walikuwa viongozi wa kwanza kutuma risala zao za rambirambi kufuatia kifo cha Bw Waititu.

Katika taarifa yake Rais Kenyatta amemtaja marehemu kama kiongozi mpenda maendeleo, mwadilifu na ambaye aliwahudumia watu wa Juja na Wakenya kwa kujitolea.

“Inasikitisha kuwa tumempoteza kiongozi mchapa kazi ambaye aliwahudumia watu wake wa Juja kwa moyo wa kujitolea,” akasema Rais Kenyatta huku akipongeza mchango wa marehemu wakati wa uhai wake katika shughuli ya utoaji uhamasisho kuhusu madhara ya saratani.

Kiongozi wa taifa ameomba Mungu aipe familia ya Bw Waititu na wakazi wa Juja nguvu wakati huu mgumu wanapoombeleza.

Kwa upande wake Bw Muturi alimtaja marehemu Waititu kama mbunge ambaye aliwatekeleza majukumu yake Bunge kwa bidii na uadilifu mkubwa.

“Nasikitika kupokea habari kuhusu kifo cha mbunge wa Juja… Natoa rambirambi zangu kwa familia, marafiki na watu wa Juja ambao aliwakilisha kwa bidii na kujitolea,” akasema Bw Muturi.

Inakumbukwa mnamo 2018 aliporejea nchini kutoka India alikopokea matibabu, Waititu aliwaambia wanahabari jinsi ugonjwa huo ulivyomwathiri kiafya na kifedha.

Alisema kuwa alitumia Sh8 milioni kama ada ya matibabu na Sh1.8 milioni kugharimia malazi kwa muda wa miezi minne akitibiwa India.

Aliongeza kuwa alipokuwa India, alipatana na Wakenya na maafisa wakuu wa serikali ambao walikuwa wameishi nchini humo wakitibiwa saratani aina mbalimbali.

“Wakenya hao walikuwa wameandamana na familia zaidi, hali ambayo iliwagharimu kiasi kikubwa cha fedha,” akasema wakati huo.

Wakati huo mbunge huyo aliahidi kuanzisha kituo cha matibabu ya saratasi katika eneobunge la Juja.

Waititu aliiinga katika siasa mnamo 2013 na akashinda kiti cha ubunge cha Juja kwa tiketi ya chama cha The National Alliance (TNA).

Alihifadhi kiti hicho katika uchaguzi mkuu wa 2017 kwa tiketi ya Jubilee.

You can share this post!

Crystal Palace wazamisha chombo cha Brighton na kumweka...

ODONGO: Kalonzo, Mudavadi na Weta wajitafutie kura