Siasa

TANZIA: Mbunge wa Matungu Justus Murunga afariki

November 15th, 2020 2 min read

NA SHABAN MAKOKHA na WANGU KANURI

Mbunge wa Matungu, Justus Murungu amefariki Jumamosi usiku alipokuwa akikimbizwa katika Hospitali ya St Mary’s mjini Mumias.

Wiki mbili zilizopita, Bw Murunga aliugua na akalazwa katika hospitali ya Aga Khan jijini Kisumu ambapo alikuwa akipokea matibabu ya ugonjwa wa kisukari na shinikizo la damu.

Mwenyekiti wa kamati ya NG-CDF, Athman Wangara alisema kuwa mbunge huyo alitolewa hospitalini Alhamisi na akawa anazidi kupata afueni nyumbani kwake Emakunda-Matungu. Mnamo usiku wa Jumamosi ya Novemba 14, alianza kupata matatizo ya kupumua.

“Alishinda siku nzima akiwapokea wageni ambao walimtakia kupona kwema na alikuwa mwenye furaha nyingi huku akiwapa matumaini waliomtembelea kwa kuwaambia kuwa anazidi kupata afueni,” akasema Wangara.

Familia yake ilisema kuwa aliwaonyesha wahandisi pahali ambapo wangejenga tanki la maji katika bustani yake kabla ya chajio. “Alipokuwa akipanda vidato, alikosa nguvu na kuzirai. Alisaidiwa na waliokuwa nyumbani huku wakikimbiza katika hospitali ya Matungu Sub-county lakini hakukuwa na mashine za oksijeni huku ikiwalazimu kumpeleka hospitali ya St Mary’s ambako alifia njiani, ” akaongeza Wangara.

Marafiki na wanafamilia walifurika kwenye mochari baada ya kusikia kifo cha mbunge wao huku majonzi na kilio kikiwajaa moyoni na machoni mwao.

Mbunge wa Mumias Mashariki, Benjamin Washiali na aliyekuwa Waziri wa Michezo, Rashid Echesa walifika mochari ambapo mwili wa Murunga ulikuwa umehifadhiwa. Bw Washiali alimuomboleza Murunga akisema kuwa mwendazake alikuwa rafiki yake wa karibu na ambaye hakujua mipaka ya uongozi wa kuwasaidia wananchi wa Matungu.

“Hivi majuzi, marehemu alikuwa amelazwa katika hospitali ya Aga Khan ambako alikuwa akitibiwa ugonjwa wa Kisukari na ugonjwa wa shinikizo la damu lakini akatolewa hospitalini akiwa mwenye siha afadhali. Yasikitisha kuwa ametuacha, ” akaongeza Washiali.

Isitoshe, Bw Washiali alisema kuwa mwili wa mwendazake utasafirishwa katika hifadhi ya mili ya Lee, Nairobi huku maziko yakipangwa.

Bw Echesa alisema kuwa ilimshtua kufahamu kifo cha Murunga. “Murunga alikuwa kiongozi mzuri na ambaye atakumbukwa kwa kuwahudumia wakazi wa Matungu. Ninawapa risala za rambirambi wakazi wa Matungu na chama cha ANC. Mungu awape nguvu mnapopambana na nyakati hizi ngumu,” akasema Echesa.

Marehemu alizaliwa mnamo 1961 na akawa kwenye kinyang’anyiro cha kiti cha ubunge cha Matungu kutoka mwaka wa 2002 lakini akawania kiti hicho Agosti 2017 katika chama cha kitaifa cha Amani Congress huku akimshinda David Were ambaye alikuwa kiongozi wa Matungu kutoka mwaka wa 2007 hadi 2013.

Viongozi kadhaa wakiwemo  Naibu Rais Dkt William Ruto, gavana wa Kakamega Wycliffe Oparanya, aliyekuwa seneta wa Kakamega Boni Khalwale, mbunge wa Khwisero Christopher Aseka na Seneta Cleophas Malala walimuomboleza Murunga.

Dkt Ruto alisema kuwa mwendazake alikuwa kiongozi mchapa-kazi na mwenye maono mengi haswa kwa wakaazi wa Matungu. “Mheshimiwa Murunga alikuwa kiongozi mpenda watu na tutaishi kukumbuka uongozi wake na alivyopenda kuwaunganisha watu wa Magharibi,” Daktari Ruto akaandika katika ukurasa wake wa kijamii.

Gavana Oparanya alisema kuwa Murunga alikuwa kiongozi mfanyakazi na aliyejitolea kwa wananchi huku akifanya kazi kwa ushirika sana ili kuboresha eneo la Matungu. “Ninahuzunika sana kwa kifo cha Murunga ambacho kimefanya Kakamega kupoteza kiongozi mwadilifu ambaye mchango wake nchini utakumbukwa. Mungu ailaze roho yake pahala pema peponi,” akasema.