Habari Mseto

TANZIA: Mchezaji Ian Waraba wa Kenya Harlequins afariki mjini Kitale

August 11th, 2020 1 min read

Na CHRIS ADUNGO

ULINGO wa raga ya Kenya umepigwa pute na kifo cha mchezaji Ian Waraba aliyeaga dunia mnamo Agosti 9, 2020 akiwa na umri wa miaka 23.

Waraba ambaye alikuwa mwanaraga wa kikosi cha Kenya Harlequins alikufa maji katika bwawa la Wamuini, Kitale, Kaunti ya Trans-Nzoia.

Kwa mujibu wa ripoti ya polisi katika Kituo cha Kiminini, Waraba alikuwa katika kundi la marafiki walioandamana naye kupiga mbizi katika bwawa hilo kabla ya mauko kumpata.

Wapiga-mbizi wa Shirika la Msalaba Mwekundu mjini Kitale waliopoa mwili wa Waraba katika bwawa hilo mnamo Jumapili ya Agosti 9, 2020.

Kwa mujibu wa Harlequins, Waraba ambaye pia aliwahi kuvalia jezi za klabu ya Vandals, alianza kuwachezea mnamo 2019 akiwa mwanaraga wa kikosi chipukizi kabla ya kujipa uhakika wa kuunga kikosi pili na hatimaye wing’a wa akiba katika kikosi cha kwanza.

Alitegemewa sana na Harlequins katika kipute cha wanaraga 11 kila upande cha kuwania ubingwa wa Eric Shirley Shield mnamo 2019.

Kakaye Waraba, Brian ambaye pia ni mchezaji wa Harlequins katika Ligi Kuu ya Kenya Cup, alisema: “Ian alithamini sana mchezo wa raga na nilimtegemea kwa mawaida kuhusu jinsi ya kujikuza kitaaluma tangu 2018.”