TANZIA: Mhariri wa zamani wa Taifa Leo afariki

Na LEONARD ONYANGO

MHARIRI msanifishaji wa zamani wa gazeti la Taifa Leo Dennis Geoffrey Mauya, maarufu Mauya Omauya, amefariki baada ya kuzimia ghafla mtaani Donholm, Nairobi.

Kulingana na jamaa zake, Mauya alizimia na kufariki papo hapo Jumatatu mchana, alipokuwa akitoka dukani, mita chache kutoka Kituo cha Polisi cha Savannah, Donholm.

Maafisa wa polisi walifika katika eneo la tukio na kupeleka mwili katika mochari ya Hospitali ya Mama Lucy Kibaki. Lakini saa chache baadaye familia iliwasili na kuhamishia mwili katika Mochari ya Chiromo.

“Nilimpigia simu Mauya lakini ikapokelewa na afisa wa polisi ambaye aliniambia kwenda katika Hospitali ya Mama Lucy Kibaki baada ya kumfahamisha kwamba nilikuwa ndugu yake,” akasema Bw Sam Kiyaka, kaka yake mwendazake.

Kulingana na Bw Kiyaka, Omauya amekuwa akiishi mtaani Zimmerman kwa muda wa miezi minne iliyopita.

“Alikuwa akiishi kwangu mtaani Zimmerman baada ya kutofautiana kidogo na mkewe. Jumatatu asubuhi aliondoka kwenda kutembelea watoto wake wawili na mkewe mtaani Donholm na baadaye alifaa kwenda katikati mwa jiji la Nairobi kununua miwani.

“Lakini hatujui ikiwa alifika au alizimia akiwa njiani kuelekea huko. Hatujui alizuru maeneo yapi kati ya saa 2.00 asubuhi na saa 1.00 mchana alipopatikana akiwa amefariki ,” akasema Bw Kiyaka.

Polisi wanashuku kuwa huenda Omauya alifariki kutokana na matatizo ya kushindwa kupumua kutokana na ugonjwa wa corona.

“Tuna hakika kwamba hakuuawa na corona kwani alidungwa chanjo ya AstraZeneca wiki mbili zilizopita,” akasema Bw Kiyaka.

Mauya alijiunga na kampuni ya Nation Media Group (NMG) kama mhariri msanifishaji wa gazeti la Taifa Leo mnamo 2007. Baada ya kufanya kazi kwa mwaka mmoja, alipata ufadhili na kwenda kusomea Masuala ya Kimataifa, Mawasiliano na Diplomasia kiwango cha Uzamili katika Chuo Kikuu cha London, Uingereza.

Baada ya kukamilisha masomo yake, Mauya alirejea tena katika kampuni ya NMG ambapo aliendelea na majukumu yake ya mhariri msanifishaji wa Taifa Leo kati ya 2012 na 2014.

Baada ya kuondoka NMG alienda kufundisha katika vyuo vikuu vya Moi, Nairobi na Karatina. Omauya amekuwa akiandika maoni ambayo yamekuwa yakichapishwa katika gazeti la Taifa Leo kila Ijumaa.

Omauya pia alikuwa mtafiti na mwandishi wa gazeti la China linaloangazia masuala ya Afrika, ‘ChinAfrica’.

Wanahabari wa gazeti la Taifa Leo, wakiongozwa na Mhariri Mkuu Peter Ngare, walimtaja Mauya kama mchapa kazi, mwaminifu, mpenda haki na mweledi wa masuala ibuka ya humu nchini na ngazi ya kimataifa.

Habari zinazohusiana na hii