Habari Mseto

Tanzia mvulana wa miaka 17 akiangamiza msichana wa miaka 7  

April 14th, 2024 1 min read

NA MWANGI MUIRURI

MWANAFUNZI wa kiume wa miaka 17 kutoka Kaunti ya Kirinyaga ametiwa mbaroni kwa madai alimuua binamuye wa kike wa miaka 7 usiku wa kuamkia Aprili 13, 2024.

Mshukiwa ambaye ni mwanafunzi wa kidato cha tatu, inasemekana alimuua msichana huyo wa darasa la saba ambaye kabla ya mauti hayo alikuwa akisomea shule ya msingi ya Rwang’ondu.

Mauaji hayo yaliripotiwa kutekelezwa katika mtaa wa Kagio na baadaye mshukiwa akatoweka.

Kwa mujibu wa kamanda wa polisi Kirinyaga Bw Andrew Naibei, mshukiwa huyo ambaye ni mwanafunzi wa Shule ya Upili ya Gathuthi-Ini alitiwa mbaroni katika Kaunti ya Kiambu alikokuwa amekimbia kutafuta hifadhi katika boma la mjomba wake.

“Alidhani angempa hifadhi lakini ndiye alipiga simu kwa maafisa wa polisi waliofika katika boma lake na kumtia mbaroni,” akasema Bw Naibei.

Kijana huyo alisemwa kuwa mapepo mbaya ya mauti ambapo pia alisikika akisema kwamba alipania kumuaa nyanya yake.

Bw Naibei alisema kwamba tayari mshukiwa huyo amesafirishwa kutoka kituo cha polisi cha Ruaka hadi kile cha Kiamaciri, Kirinyaga.

“Tutamwasilisha mahakamani mnamo Jumatatu (Aprili 15, 2024) ambapo tutaomba muda zaidi kukamilisha uchunguzi na ikiwa ushahidi utatosha, tumshtaki kwa mauaji,” akasema.

Bw Naibei alisema kwamba upasuaji wa mwili ndio utabaini jinsi mwathiriwa alipoteza uhai wake huku uchunguzi zaidi ukiweka wazi njama hiyo ilivyotekelezwa.

[email protected]