Habari

TANZIA: Mwanafasihi mtajika Prof Ken Walibora afariki

April 15th, 2020 1 min read

NA FAUSTINE NGILA

HUZUNI imetanda miongoni mwa wapenzi wa lugha ya Kiswahili na fasihi kwa jumla baada ya mwandishi maarufu Prof Ken Walibora Waliaula kufariki.

Taifa Leo Dijitali imethibitisha Jumatano asubuhi kuwa mwandishi huyo wa Siku Njema, Nasikia Sauti ya Mama na Kidagaa Kimemwozea alifariki baada ya kugongwa na matatu katika barabara ya Landhies, jijini Nairobi hapo Ijumaa.

“Kwa sasa nipo katika mochari ya Hospitali Kuu ya Kenyatta. Ni kweli kwamba profesa ametuacha,” alisema mhariri wa makala katika gazeti la Taifa Leo Bw Stephen Musamali.

Mwandishi huyo amekuwa akitafutwa tangu atoweke Ijumaa iliyopita, hali iliyozua hofu mitandaoni kuwa huenda alikuwa ashafariki.

Prof Walibora ambaye kwa muda mrefu alikuwa mwanahabari aliyependa kusoma habari za lugha ya Kiswahili, pia alisimamia ubora wa lugha hiyo katika kampuni ya Nation Media Group (NMG) hadi miaka mitatu iliyopita.

Mhariri Mkuu wa gazeti hilo Bw Peter Ngare alisema ni siku ya huzuni kwa waandishi na wapenzi wa Kiswahili waliofurahia kusoma makala yake ya kila Jumatano – Kina cha Fikra, Kauli ya Walibora, yaliyowakosoa kuhusu matumizi ya lugha hiyo.

“Tuombe Mungu atuepushe na hili janga la matatu. Prof Walibora ni mtu wa nne aliye na uhusiano na NMG kuuawa na matatu chini ya muda wa miezi miwili,” alisema.

Mhariri wa habari katika gazeti la Kiswahili Bw Juma Namlola aliyetangamana naye katika ulingo wa uandishi wa riwaya alisema ni huzuni kubwa Kenya kupoteza msomi kama huyo.

“Ni huzuni kubwa. Daima alikuwa akiniita “mwalimu” nami nikimwita “mtoto wa mwalimu”. Yeye na Bitugi Matundura hawakukosa kuniuliza nimefikisha vitabu vingapi. Kalamu ya Mungu, wino wake haufutiki!,” alisema.