Habari za Kitaifa

TANZIA: Mwanahabari Fatma Rajab Ali wa Mo Radio aaga dunia

January 6th, 2024 2 min read

NA FARHIYA HUSSEIN

SIKU moja tu baada ya wanahabari katika Kaunti ya Mombasa kuungana na familia ya mwenzao aliyehitaji msaada wa kifedha kufanikisha matibabu, mgonjwa huyo ameaga dunia.

Fatma Rajab Ali aliaga dunia Jumamosi alipokuwa akitibiwa katika kitengo cha matibabu ya wagonjwa mahututi katika Hospitali ya Rufaa ya Pwani ambayo wengi wanaifahamu kama Coast General.

Baba yake, Ali Rajab, alifichua kuwa Fatma alizaliwa na matatizo ya moyo, ambayo yaligunduliwa alipofikisha umri wa miaka 14 tu.

Valvu ya moyo wake ilikuwa imeharibika, ikisababisha matatizo ya moyo ya mara kwa mara.

Mwaka 2014, Fatma alifanyiwa upasuaji wa kubadilisha valvu nchini India, ambapo valvu yake ya awali ilibadilishwa.

Hata hivyo, matatizo yalijitokeza tena kwani valvu iliyowekwa mpya ilikwama kwa muda.

“Kwa umri wa miaka 26, alianza kupata matatizo makubwa tena,” alisema babake Bw Rajab.

Fatma, alijulikana kwa kazi yake katika Radio Salaam na Mo Radio.

Alikuwa akiendelea vizuri chini ya uangalizi wa daktari wake maalum wa moyo hadi alipokumbana na kifo chake.

Shangazi yake, Bi Mwanathuma Abdalla, aliambia Taifa Leo kuwa baada ya kurudi kutoka India mwaka wa 2014, mwezi mmoja baadaye Fatma alikumbana na maumivu ya tumbo, ambayo yalisababisha ugunduzi na kuondolewa kwa mmojawapo wa mifuko ya mayai ya uzazi kupitia upasuaji.

Mnamo Jumatano wiki hii, Fatma alipata tena maumivu, akaanza kutapika damu, na akapelekwa haraka hospitalini.

Kabla ya kifo chake, familia yake ilikuwa imeomba msaada kugharimia upasuaji ambao mwanahabari huyo alihitaji kufanyiwa kubadilisha valvu yake.

“Akiwa na gharama za dawa zinazopita Sh6,000 na hitaji la upasuaji wa haraka, tunatafuta msaada wowote,” alisema Bi Abdalla wakati huo.

Kwa ishara ya mshikamano, waandishi wa habari wa Mombasa walikutana Ijumaa ambapo baadhi yao walijitolea kuchangia damu, huku wengine wakichangia kadri walivyoweza.

Daktari wa Kitengo cha Matibabu ya Wagonjwa Mahututi, Dkt Hassan Ali, alikuwa amethibitisha hali ya hatari ya Fatma alipowasili, akielezea dalili zake za maumivu ya tumbo na kutapika damu.

Gavana wa Mombasa Abdulswamad Nassir ni miongoni mwa viongozi ambao wametuma risala za rambirambi kwa familia ya marehemu, ambapo ameahidi kufuta bili ya matibabu.

Fatma atazikwa Jumapili.