Tanzia: Mwanamume amuua nduguye kabla kujitia kitanzi

Tanzia: Mwanamume amuua nduguye kabla kujitia kitanzi

NA NYABOGA KIAGE

POLISI eneo la Mwingi wameanzisha uchunguzi kufuatia kisa cha mwanamume aliyemuua ndugu yake, kabla ya kujitia kitanzi.

Kulingana na wakazi, wawili hao walikuwa wakifanya kazi pamoja shambani kabla ugomvi kuzuka.

Kilichoanza kama mzaha kiliishia kuwa vita na kusababisha maafa.

Bw Peter Mwenda, ambaye ni jirani alisema aliskia mayowe kisha akakimbia shambani kubaini kilichokuwa kikiendelea ambapo alipata mmoja wao akivuja damu.

“Tulimpata akitokwa na damu, ndiposa tukachukua hatua kumkimbiza hospitalini. Alifariki hata kabla kumfikisha,” Mwenda alisema.

Akielezea kushangazwa na tukio hilo, mkazi huyo alisema wawili hao wamekuwa wakiishi kwa amani.

Mkazi mwingine, Bw Ben Kilunda, alisema kwamba anashuku huenda jamaa aliyejitia kitanzi alizongwa na msongo wa mawazo.

Alitorokea katika nyumba yake, baada ya kutekeleza mauaji na kujitia kitanzi.

“Alijifungia kwenye nyumba yake, na tulipochungulia tukaona amejitia kitanzi. Linaonekana kama tukio la kishetani,” Kilunda akasema.

Akithibitisha mkasa huo, mkuu wa polisi eneo la Mwingi Bw Kyalo Kazungu alisema uchunguzi umeanzishwa kubaini kiini.

“Tunaomba wakazi wawe na subira uchunguzi ufanyike. Hata hivyo, inaonekana aliyejitia kitanzi alimkata nduguye kwa panga,” afisa huyo akasema.

  • Tags

You can share this post!

Misimamo mikali yazuia majadiliano ya RaiRuto

Wakenya puuzeni hiyo likizo mwitu ya Raila, asema Gachagua

T L