Kimataifa

TANZIA: Mwanamuziki Aurlus Mabele afariki

March 20th, 2020 1 min read

Na MASHIRIKA

PARIS, Ufaransa

MWANAMUZIKI mashuhuri kutoka Congo Brazzaville Aurlus Mabele alifariki Alhamisi usiku katika hospitali jijini Paris alipokuwa amelazwa.

Mabele aliyekumbana na kifo akiwa na umri wa miaka 67 alikuwa na virusi vya corona kando na kuathiriwa na saratani.

Mwanamziki mwenzake Nyboma Mwandido alithibitisha tanzia hiyo akisema ilithibitishwa kuwa aliugua Homa ya Corona mnamo Machi 19.

Kabla ya kufariki kwake, alikuwa anaishi katika Paris nchini Ufaransa.

“Mabele alilazwa hospitalini Alhamisi jioni alipopimwa na kupatikana na virusi vya corona,” alisema.

Alitambulika kwa kuanzisha nyimbo za Soukous, jambo ambalo lilifanya aitwe jina la utani la King of Soukous.

Mnamo 1974 alianzisha bendi pamoja na wanamziki wenzake Jean Baron, Pedro Wapechkado na Mar Cacharel, bendi hiyo ilijulikana kama Les Ndimbola Lokole.

Baadaye, aliwaunga mkono Mar Cacharel na Diblo Dibala mnamo 1986 na kuanza bendi nyingine.

Waliimba nyimbo maarufu kama Extra Ball, Embargo na Liste Rouge.

Mabele alizaliwa mnamo 1953 katika mji wa Aurelien Miatsonama mkoa wa Brazzaville ulio Congo.