TANZIA: Mwanamuziki Muriithi John Walker afariki baada ya kuugua ghafla

TANZIA: Mwanamuziki Muriithi John Walker afariki baada ya kuugua ghafla

Na MWANGI MUIRURI

MKUKI wa mauti umetembelea safu ya utumbuizaji Mlima Kenya na kuilenga roho ya Muriithi John Walker ambaye aliaga dunia alasiri ya Ijumaa baada ya kuugua ghafla.

Walker ni miongoni mwa wanamuziki wa kizazi cha 2000 ambacho kilileta ubunifu wa hali ya juu wa jinsi upigaji gitaa unavyoweza kutumika kuchachawisha umma katika maeneo ya burudani ikitumika na mwimbaji kujiongoza yeye mwenyewe katika kile kinajulikana kama One-Man-Guitarist.

Kwa mujibu wa mwenyekiti wa muungano wa Wanamuziki chini ya Ushirika wao wa Talented Musicians and Composers Organisation (Tamco) Bw Epha Maina, wapenzi wa burudani haswa Mlima Kenya walimpoteza Bw Walker alipokuwa akipelekwa hospitalini.

“Ni suala lililo na tanzia kuu kwa kuwa Bw Walker hakuwa na matatizo ya kiafya ambayo yanaweza yakawa yalituandaa kukubali kuondoka kwake duniani. Lakini kilicho wazi sasa ni kuwa Bw Walker amefariki na kwa sasa ameanza maisha yake ya utulivu wa milele,” Bw Maina akaambia Taifa Leo.

Mwili wake ulisafirishwa kuhifadhiwa katika mochari ya Chuo Kikuu cha Kenyatta.

Bw Maina alisema kuwa Bw Walker alipelekwa katika hospitali moja ya viunga vya Kaunti ya Nairobi na wakaagiza ahamishiwe nyingine wakati ilibainika amezidiwa na kabla hata ya kufikishwa kwa lango la hospitali hiyo ya pili, akasalimu amri ya mkuki wa mauti.

Bw Walker alikuwa na ubunifu wa kipekee wa kutunga nyimbo zake kwa lugha ya Gikuyu zilizopata umaarufu katika maeneo ya burudani kote nchini.

Mada zake zilikuwa na ubunifu wa kipekee na ambazo zililenga kuhamasisha kuhusu masuala nyeti ya kijamii yakiwemo ugonjwa hatari wa Ukimwi, maamuzi kuhusu ngono, na tamaa ya kuchovyachovya asali mizingani katika anasa za ulevi.

Mwendazake anaweza akatajwa kama mshauri, mwalimu wa walevi hasa kwa wanaume ambao huwa na mazoea ya kujisahau na kujiachilia kwa hatari za anasa ndani ya mtindi.

Katika ngoma yake inayofahamika kama ‘Uhiki Wi Murio’ (Harusi ni Tamu), Bw Walker huwashauri wanaume kwa wake walenge kujiingiza katika umoja wa ndoa ya wawili wa jinsia tofauti na wazindue ujenzi wa familia badala ya kuingia kwa mang’weni kusaka “utamu wa ndoa kwa njia ya vipimo.”

Alitoa ngoma nyingine inayojulikana kama ‘Nuu Ui Handu Kiri?’ (Nani Anajua Kinaweza Kuatikana Wapi?) ambapo kwa ustadi na ustaarabu mkuu Bw Walker huficha nia kuu ya uchafu ndani ya wimbo huo wa kuuliza huo mzinga ambao huchachawisha wanaume wakiusaka ndani ya kila sketi hupatikana wapi.

Kwa wimbo wake yeye Bw Walker anawashauri wanaume waende polepole wasiishie kujikwaa katika soko hilo la uzinifu “kwa kuwa mnanunua kile huwezi kufungiwa uende nacho nyumbani” huku akisema yeye mwenyewe ameridhika katika ndoa yake na hawezi kwenda kwa soko ambayo hakuna ile bidhaa imewekwa wazi wengi wachambue, waone kwa macho na waguze kwa mkono na hata kunusa hadharani kwa kuwa ni soko…

Bw Walker pia alikuwa na mazoea ya kulinganisha hali kwa njia ya ubunifu ambapo katika ngoma yake inayojulikana kama Nyau Iriaga Mbia (Paka Hula Panya) anasema kuwa kila kitu huwa na nia yake…kila ugonjwa uko na dawa yake “jinsi vile kunao wanyama ambao kwa lishe hula kuku, panya huliwa na paka huku nayo kiu ya mapenzi niliyo nayo ikiwa tu inakuhitaji wewe…” Sema mistari ya kuwachachawisha warembo (hata ikiwa wengi husema mbinu ya aina hiyo inaweza tu ikafanya kazi mashambani kwa kuwa Jijini lugha ni pesa wala sio mbinu ya kuanza hadithi za panya na paka, wanyama na kuku au kiu na mapenzi…

Bw Walker pia alisema kwa wimbo wake unaojulikana kama ‘Thutha Mwega’ yaani Makalio Mazuri, ambapo anadunisha raha ya wenye mazoea ya kutamani kisirisiri mtaani wakisema “kula kwa macho” ambapo mrembo akipita tu macho ya wengi wa wanaume huangalia makalio hasa yale ya kutikisika ndani ya nguo kwa kila mpigo wa matembezi.

Mchukie au umpende Bw Walker, kwa sasa hatajali ashaenda zake na harudi, alisema makalio mazuri tu ni ya kuku au ya mbuzi kwa kuwa yanaweza yakageuzwa kitoweo cha mlo, hayo mengine yakiwa ni ubunifu wako wa tabia mbaya na mtazamo wa kimwili ambao haukufai kwa lolote.

Hiyo tu ni mifano na ukitaka zaidi, wewe enda kwa mitandao na upige mbizi ya utafiti ukisaka tu jina “Muriithi John Walker” na ngoma zake zitajitokeza wazi uzichambue na kile utakumbana nacho kwanza ni jinsi alipendwa katika safu ya burudani kwa utathimini wa manguvu ya kunengua viuno yanayotumika katika jukwaa anapoimba.

Mzawa wa Kijiji cha Thumaita katika Kaunti ya Kirinyaga, ametajwa na wengi kama “nguzo muhimu ya usanii Mlima Kenya.”

Alitajwa kuwa mkarimu, mpenda watu na aliyekuwa na familia changa ambapo binti yake kifungua mimba alikuwa anatarajia kuufanya mtihani wake wa darasa la nane mwezi huu.

Mengi yanaweza yakaandikwa kumhusu, akichambuliwa kwa sifa au kudunishwa…lakini aibu pengine ikiwa hilo halikufanyika akiwa na uhai wake ndio achangie na pia yeye ajisome kujihusu na afurahie pia…hii ikiwa ndio hali ya unafiki wa wengi wetu, kumlimbikizia sifa akiwa ashaenda lakini wema huo hatuutoi mlengwa akiwa hai.

Cha mno sasa ni yote hayo yakiwa ni tisa, la kumi ni dua tu Mungu aipe roho yake amani, hata ikiwa tena Maulana akiwa ndiye muumba na mmiliki wa nafsi na uhai ndiye ajuaye hukumu yake kwa kila mmoja wetu kwamba itakuwa gani mbele ya kiti cha enzi.

Lakini uhamasisho mkuu, kwa mujibu wa maisha aliyoishi Bw Walker, ni tenda wema, ng’ang’ana kujitambua na kujiimarisha na ujitegemee mwenyewe kujipa raha na utulivu maishani na uwe na bidii ya riziki na hayo mengine Mungu akitembelea waja wake atakuzidishia akikubariki.

Safiri salama Bw Walker uliyejulikana kwa tabasamu ya uwazi, mtindo wa nywele wa kunyolewa boksi na ‘uchawi wa kucheza gitaa’ huku umbo ukiwa na unene wa baunsa.

You can share this post!

Newcastle United na Aston Villa waridhika na sare katika...

Vinara wa EPL wanataka mashabiki 10,000 kuruhusiwa...