Michezo

TANZIA: Mwendwa na Nyamweya wamwomboleza Rais wa zamani wa FKF, Mohammed Hatimy

November 15th, 2020 1 min read

Na CHRIS ADUNGO

RAIS wa Shirikisho la Soka la Kenya (FKF), Nick Mwendwa na mtangulizi wake Sam Nyamweya, ni miongoni mwa Wakenya ambao wamemwomboleza kiongozi Mohammed ‘Babady’ Hatimy aliyeaga dunia mnamo Novemba 14, 2020 jijini Mombasa.

Hatimy alifariki katika hospitali moja jijini Mombasa baada ya kupata tatizo linalohusiana na virusi vya corona. Hadi kuaga kwake, alikuwa amelazwa katika kitengo cha wagonjwa mahututi kwa wiki moja katika hospitali hiyo.

Hatimy aliwahi kuwa kinara wa FKF ambapo alishikilia wadhifa wa urais wa shirikisho hilo kati ya 2005 na 2011.

“Kifo cha Hatimy ni pigo kubwa kwa familia yake, familia yote ya soka ya Kenya na taifa zima. Alikuwa kiongozi shupavu aliyejitolea kufanya kazi yake kwa uadilifu mkubwa. Mchango wake katika tasnia ya soka ilikuwa kubwa na maendeleo aliyoyaleta katika enzi yake ya uongozi bado yanahisika hadi leo. Tumepoteza pakubwa,” akasema Mwendwa.

“Nilifanya kazi na Hatimy kwa muda mrefu. Aliniachia mamlaka ya uongozi katika FKF kwa amani niliposhinda uchaguzi wa shirikisho hilo mnamo 2011. Alithamini na kuchangamkia sana masuala ya soka na alijitolea kwa hali na mali kutetea makuzi ya mchezo huo ndani na nje ya nchi,” akasema Nyamweya.

“Tulikuwa wepesi wa kushauriana katika masuala mengi kuhusu soka na alifurahia sana kuona timu ya taifa ya Harambee Stars ikitamba katika ulingo wa kimataifa,” akasema makamu rais wa zamani wa FKF, Twaha Mbarak.

Hatimu aliwahi pia kuwa diwani mteule katika Kaunti ya Mombasa na mwenyekiti wa masuala ya fedha katika Chama cha kisiasa cha Orange Democratic Movement (ODM), Kaunti ya Mombasa.

“Moyo wa mtu mwenye roho safi kabisa umeacha kupiga. Kiongozi aliyekuwa mtu wa watu na kigogo wa siasa ametuacha. Familia pana ya ODM imepoteza shujaa na kinara muadlifu. Tunaitakia familia faraja na subira. Tutakukosa kiongozi,” ikasema sehemu ya taarifa iliyotolewa na ODM.

Hatimy alizikwa saa kamili mnamo Novemba 14, 2020 katika Kaunti ya Mombasa.