TANZIA: Simeon Nyachae afariki

TANZIA: Simeon Nyachae afariki

Na CHARLES WASONGA

ALIYEKUWA Waziri wa Fedha na Mbunge wa Nyaribari Chache, Bw Simeon Nyachae amefariki, familia yake imetangaza rasmi kwenye taarifa Jumatatu, Februari 1, 2021.

Familia hiyo imesema Mzee Nyachae, 88, alifariki alipokuwa akipokea matibabu katika Hospitali ya Nairobi.

Mwendazake ambaye pia alihudumu kama afisa wa utawala katika serikali ya Mzee Jomo Kenyatta na marehemu Daniel Moi, alizaliwa mnamo Februari 6, 1932, akiwa mwana wa chifu wa enzi za ukoloni, Musa Nyandusi

Nyachae alisomea katika Shule ya Kanisa la Kiadventista ya Nyanchwa hadi 1941 kisha akajiunga na Shule ya Upili ya Kereri Intermediate.

Mnamo 1949 alijiunga na Shule ya Upili ya Kisii, wakati huo ikiitwa Kisii Government African School, ambako alikamilisha masomo yake ya kiwango cha ‘A’ Level.

Baadaye alijiunga na Chuo cha South Devon Technical College na kile cha Churchill College jijini Cambridge, Uingereza kwa elimu ya juu.

Mnamo 1954 aliajiriwa kama karani katika kambi ya chifu (babake) na miaka sita baadaye akahamishwa hadi tarafa ya Kangundo kuhudumu kama Mkuu wa Tarafa (DO).

Mnamo 1963 aliteuliwa kuwa Mkuu wa Wilaya na baadaye akapandishwa cheo hadi kuwa Mkuu wa Mkoa, wadhifa aliohudumu kuanzia 1965 hadi 1979.

Nyachae alihudumu kama Mbunge wa Nyaribari Chache kuanzia 1992, utawala wa vyama vingi uliporejeshwa nchini. Ni wakati huo ambapo alihudumu kama waziri katika wizara za Kilimo na Fedha, chini ya Utawala wa Daniel Moi.

You can share this post!

Wakazi wafurahia corona kupunguza ulevi vijijini

Aibu wabunge wakilimana makonde mazishini