Habari

TANZIA: Viongozi wamtumia Khalwale salamu za pole kwa kumpoteza mke

October 5th, 2019 1 min read

NA MARY WANGARI

WANASIASA mbalimbali wakiongozwa na Naibu Rais Dkt William Ruto, wameungana Jumamosi kumfariji aliyekuwa Seneta wa Kaunti ya Kakamega Dkt Boni Khalwale, kufuatia kifo cha mke wake wa kwanza Bi Adelaide Khalwale, aliyefariki kutokana na saratani.

Bi Khalwale alifariki Jumamosi asubuhi akiwa nyumbani kwake Malinya, eneobunge la Ikolomani, baada ya kuugua kwa muda mrefu.

Mwili wake ulipelekwa katika mochari ya Hospitali ya St Elizabeth Mukumu.

Dkt Khalwale aliyezidiwa na majonzi, alijitosa katika ukurasa wa mojawapo ya akaunti zake za mitandao ya kijamii kutangaza kifo cha mkewe.

“Asubuhi yenye huzuni. Kifo kimenipokonya mke wangu wa kwanza,” aliandika Dkt Khalwale.

Viongozi wakiwemo Dkt Ruto na kiongozi wa ODM Raila Odinga, walituma salamu za pole wakimfariji.

“Salamu za pole ziendee familia na marafiki wa mheshimiwa Boni Khalwle kwa kumpoteza mkeo, Bi Adelaide. Mama Adelaide alikuwa nguzo maishani mwako, mkarimu na mwenye moyo safi. Tunajali na kuombea wapendwa wake. Lala salama,” alisema Naibu Rais.

Naye kiongozi wa ODM alikuwa na pole zake kwa Khalwale.

“Naomba upokee salamu zangu za pole; kwako na familia yako yote kufuatia kifo cha mkeo mpendwa Bi Adelaide. Mola na akupe nguvu kipindi hiki kigumu,” aliandika Raila.

Wanasiasa wengineo maarufu wakiwemo maseneta Moses Wetang’ula, Kipchumba Murkomen, Katibu Mkuu wa ODM, Edwin Sifuna pia hawakuachwa nyuma kumfariji Bw Khalwale.

Hadi kufikia kifo chake, Bi Khalwale alikuwa mfanyakazi wa Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia cha Masinde Muliro (MMUST).