Tapeli mkubwa wa Showbiz Wilkins Fadhili acheza kama yeye tena

Tapeli mkubwa wa Showbiz Wilkins Fadhili acheza kama yeye tena

NA TOM MATIKO

WAKATI mwingine mimi hushindwa kuelewa kabisa Wakenya tunaishi katika sayari ipi. Juzi tena kumezuka stori kuhusu tapeli mkubwa wa Showbiz yetu kwa jina Wilkins Fadhili.

Jamaa anadaiwa kumtapeli msanii chipukizi anayekuja vizuri Trio Mio zaidi ya Sh100, 000. Huyu dogo Trio ana umri wa miaka 16 kama sijakosea na ameingia kwenye gemu ya muziki mwaka uliopita. Hiti iliyomtambulisha na kumpa umaarufu ni ile kazi yake ya Cheza Kama Wewe.

Kando na huyu dogo, huyu Wilkins pia anadaiwa kumwosha mmoja kati ya mabloga wanaofanya vizuri nchini Suzie Wokabi. Wokabi ni modo aliyejikita zaidi kwenye masuala ya urembaji na vipodozi.

Huyu binti ni msomi kweli kweli. Ana shahada kwenye masuala ya kidiplomasia na pia kasomea masuala ya urembaji kule Los Angeles. Ndiye mwasisi wa SuzieBeauty.

Amekuwa akifanya vizuri kwenye tasnia ya ulimbwende na fasheni hapa nchini. Ni mrembo aliyechanuka, kazunguka dunia na kuona mengi. Nashindwa kuelea vipi huyu mshamba aliweza kumtapeli. Mwonekano wake sio wa mtu mwaminifu. Hata ikiwa hujawahi kukutana naye na ikatokea fursa hiyo, nafsi yako itaganda kumwamini.

Sijui kabisa ni vipi aliweza kuwaingiza boksi Wokabi na Trio. Stori ya Trio kaianika mamake mzazi Irma Sakwa aliyetangaza kuwa mwanawe amekatiza mahusiano na Wilkins kama meneja wake.

Wokabi naye anadai kuwa ‘gathee’ alihepa na baadhi ya rekodi zake alizokusudia kupeperusha kwenye ‘Podcast’ yake. Alikuwa meneja wa ‘Podcast’ hiyo ya Wokabi.

Kulingana naye walikuwa wameshuti video kibao zilizopaswa kupakiwa ila sasa jamaa kaingia nazo mitini na anazitumia kuwatoanisha hela wateja wa SuzieBeauty.Kilichonisinya ni taarifa aliyoitoa Wokabi akifafanua namna Wilkins alivyomtapeli video hizo.

Kwenye taarifa yake anaanza kwa kusema; “Hii ni taarifa kwa umma. Chukueni tahadhari dhidi ya Wilkins Fadhili Odinga, kafanya tena mambo yake na nahisi ni sahihi kwangu mimi kumwanika huyu tapeli sugu…”

Sasa hapo ndipo narudi kwenye sentensi ya kwanza ya makala haya. Sielewi Wakenya wakati mwingine huwa tunaishi kwa sayari ipi.Hatua ya Wokabi kukiri kwamba Wilkins karudia tena tabia zake za kitapeli ni thibitisho kwamba, tayari alikuwa anayo historia za huyu tapeli wa mjini anayemiliki Wilkins Studio Agency na Wilkins Podcast.

Sio mara ya kwanza kusikia madai ya utapeli dhidi yake lakini bado aliamua kumwamini na kumpa kazi ya kuwa meneja wa ‘podcast’ yake. Inashangaza.

Kwake Trio, masikitiko yangu ni kwamba hivi ni vipi walishindwa kabisa kumpiga msasa na kufuatilia stori zake kabla ya kumfanya meneja!Ikumbukwe kuwa 2019, mwanahabari maarufu wa BBC Larry Madowo alitishia kumfungulia mashtaka bwana tapeli huyu baada yake kugundua kwamba jamaa alikuwa akitumia jina lake kuwatapeli Wakenya.

Baada ya Madowo, wakatokea maceleb kibao akiwemo Edith Kimani, Victoria Rubadiri na Adelle Onyango waliodai kuwa jamaa amekuwa akitumia majina na brandi zao kuwaosha Wakenya vile vile.

Alichokuwa akifanya ni kujipendekeza kwa mastaa hawa, kisha anapiga nao picha kwenye mapozi ya namna ya kikazi halafu anatumia picha hizo kutapeli watu.Baada ya kuanikwa jamaa alitishia kujitoa maisha.

Kumbe kama vile ilikuwa ni mlango wake wa kuhepa ngori. Toka alipotoa taarifa hiyo, watu waliacha kumwandama na jamaa akaendelea na maisha yake. Sasa tena huyo kaibuka.

Sitashangaa kusikia tena katapeli baada ya mwaka. Na watakaotapeliwa ni nyie Wakenya tu ambao kwa sasa mpo bize kumkashifu kama tu Wokabi aliyekuwa tayari anazo data zake za utapeli lakini bado akawa zuzu na kumpa kazi.

You can share this post!

Nairobi kunoma, asimulia rapa Majirani

Makanisa yachomwa, ukuta wapakwa kinyesi Kisii