Habari za Kitaifa

Tarajieni mvua nyingi Machi hadi Mei – MET

March 1st, 2024 1 min read

NA KENYA NEWS AGENCY

IDARA ya Utabiri wa Hali ya Hewa nchini imetoa tahadhari kuhusu kuongezeka kwa mvua inayotarajiwa kote nchini msimu wa masika wa Machi-Mei ikitaka serikali kuweka matayarisho na suluhu mbadala za kupunguza vifo na uharibifu wakati wa mafuriko.

Utabiri huo unaonyesha kuwa mvua inatarajiwa katika kaunti zilizo karibu na Ziwa Victoria, Bonde la Ufa, Kati, Nairobi, Kaskazini-Mashariki na Kusini-Mashariki.

Kulingana na Mkurugenzi Dkt David Gikungu, viwango vya juu vya mvua vinatarajiwa kufikia kilele Aprili. Mvua hiyo itaathiri sekta za Afya, Kilimo na Nishati miongoni mwa nyingine.

“Kama idara, tutaendelea kutoa taarifa kuhusu utabiri wa mvua ili kufahamisha matayarisho na hatua zinazofaa kutoka kwa wakulima hadi kwa serikali,” alisema Dkt Gikungu.

Dkt Ayub Manya kutoka Wizara ya Afya alisema mvua hiyo itapunguza utapiamlo kutokana na chakula cha kutosha ila pia inaweza kuongeza milipuko ya magonjwa.

Dkt Manya ametaka kuwepo kwa matayarisho ili kukabiliana na magonjwa ibuka yatokanayo na maji kama vile malaria na kuhara kwa kusaidia vituo vya afya vya jamii pamoja na upatikanaji wa vyandarua na dawa.

Alisisitiza kuwa Wizara ya Afya inaendelea kuweka mikakati na kukagua maeneo yenye watu wengi nchini kote ambayo hukumbwa na mafuriko ili kudhibiti kuibuka kwa magonjwa na milipuko.