Michezo

Tarehe mpya za michuano ya Kombe la FA zatolewa

May 31st, 2020 1 min read

Na CHRIS ADUNGO

ROBO-FAINALI za mechi za kuwania ubingwa wa Kombe la FA msimu huu sasa zitaandaliwa wikendi ya Juni 27-28, 2020 huku fainali ikiratibiwa kutandazwa Jumamosi ya Agosti 1.

Afisa Mkuu Mtendaji wa FA, Mark Bullingham hata hivyo amesisitiza kwamba kusakatwa kwa michuano hiyo jinsi ilivyopangwa kutategemea iwapo kanuni zote za afya zilizowekwa katika juhudi za kukabiliana na janga la corona zitazingatiwa na wahusika.

Mahali na wakati kamili wa kupigwa kwa mechi hizo utatolewa baadaye wiki ijayo.

Mechi za nusu-fainali za kipute hicho zitaskatwa kati ya Julai 18-19, 2020.

Mnamo Alhamisi iliyopita, vinara wa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) walifichua mipango ya kurejelewa kwa kivumbi hicho msimu huu mnamo Juni 17 kwa matumaini ya mechi zote 92 zilizosalia kusakatwa kufikia mwanzoni mwa Agosti 2020.

“Afya na maslahi ya wachezaji, maafisa wa vikosi na washikadau wote wengine ndiyo muhimu zaidi katika masuala tunayoyapa kipaumbele kwa sasa,” akatanguliza Bullingham.

“Kombe la FA ni sehemu muhimu katika kalenda ya soka ya Uingereza kwa takriban miaka 150 sasa. Tungependa kushukuru sana vinara wa EPL na wachezaji wao kwa kuafikiana kuhusu mipango ya kuratibu upya mechi zote zilizokuwa zimesalia kabla ya mkurupuko wa virusi vya corona,” akasema.

Droo ya robo-fainali za Kombe la FA ilifanyika mnao Machi 9, 2020. Leicester City watakuwa wenyeji wa Chelsea ugani King Power, Manchester City wawaendee Newcastle United uwanjani St James’ Park nao Sheffield United wakwaruzane na Arsenal ugani Bramall Lane. Norwich City watakuwa wenyeji wa Manchester United uwanjani Carrow Road.

DROO YA ROBO-FAINALI ZA FA:

Leicester City na Chelsea

Newcastle United na Manchester City

Sheffield United na Arsenal

Norwich City na Manchester United