Makala

Taswira ya ukora wa polisi ulioishia mauti ya mshukiwa katika seli Maragua yaibuka

April 24th, 2019 2 min read

Na MWANGI MUIRURI

IMEANZA kuibuka kuwa Hamuel Muguro Ngugi aliyeaga dunia katika seli za polisi za Stesheni ya Maragua alijipata katika mtego wa uhasama kati ya mwajiri wake na maafisa wa polisi.

Amezikwa Jumatano.

Uhasama huo unasemwa kuwa hata baada ya kukamatwa, kuna maafisa waliodai hongo ya Sh100,000 ili mambo yatulie ndani ya sakata hiyo na baada ya kukataa kuitoa hongo hiyo, mambo yakazidi unga kiasi cha kuishia mauti ndani ya seli.

Taarifa za uchunguzi ambazo zinaendelea kuandikishwa na mamlaka ya kumulika utendakazi wa maafisa wa Polisi (IPOA) zimebaini kuwa kuna afisa mmoja mkuu katika kituo hicho aliyekuwa amesisitiza kumwadhibu mumilki wa baa ya Starehe ambayo marehemu alikuwa mhudumu.

Kwa mujibu wa taarifa ya Bw Wairegi Cheki, maafisa hao walikuwa wameripoti katika biashara hiyo ya pombe asubuhi ya Jumamosi hiyo wakidai hongo lakini wakanyimwa.

“Wakiondoka, waliapa kuwa wangetupa adhabu ya kuwapuuza. Na ndipo usiku huo walituvamia mwendo wa saa tano na dakika tano tukiwa hatuna wateja bali tulikuwa sisi waajiriwa wa baa hiyo tukifunga madirisha ndio tuelekee zetu manyumbani,” akasema Cheki.

Anasema kuwa maafisa hao walipuuza biashara haramu ya uuzaji chang’aa iliyokuwa ikiendelezwa kando mwa baa hiyo na ambayo ilikuwa ikiuzwa na genge la vijana waliokuwa wamejihami kwa mapanga na mipini, lakini wakavamia baa ambayo ilikuwa imefunga kazi kwa mujibu wa sheria.

“Maafisa hao pia walipuuza ushauri kuwa Bw Muguro alikuwa na matatizo ya kimwili na haikukuwa na busara yoyote ya kumtia mbaroni bali hata angeandikiwa bodi ili awe huru.”

Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Tume ya Huduma ya Polisi Bw Eliud Ndung’u Kinuthia, ni haki ya kila mshukiwa wa makosa madogo kupewa bodi wakati wowote ndani ya kituo cha polisi na ikiwa makosa ambayo amekamatiwa hayazui kifungo cha zaidi ya miezi sita gerezani, hufai kufungiwa ndani ya seli.

Anasema kuwa huo ni mwelekeo ambao umetolewa na NPSC na pia afisi ya Inspekta Mkuu wa Polisi (IG) Hilary Mutyambai.

“Hakukuwa na sababu yoyote ya kukataa kumpa bondi mshukiwa huyo kwa kuwa wenzake watatu walikuwa wametiwa mbaroni huku mwajiri wao, Kinuthia Ngai akijitolea kuwa mdhamini wa mshukiwa huyo akiwa huru,” anasema wakili Geoffrey Kahuthu wa mahakama kuu.

Shida ni kuwa hata baada ya mshukiwa huyo kuaga dunia akiwa ndani ya seli hizo, na ambapo mashahidi wanashikilia kuwa mito yao ya kusaka usaidizi ilipuuzwa na waliokuwa katika kituo hicho usiku huo wa mauti, wenzake watatu walifikishwa mahakamani na kushtakiwa.

Ni mashtaka ambayo hata kamanda wa polisi wa Murang’a, Josephat Kinyua anataja kuwa yenye shaka kuu.

Ikifahamika vyema kuwa washukiwa hao wote walikuwa wahudumu wa baa hiyo, makaratasi ya mashtaka yaliwaorodhesha watatu kuwa wateja wa baa hiyo na mmoja akiwa muuzaji.

“Marehemu Muguro, Waithaka Njeri na Kamari wakieleweka vizuri kuwa walikuwa wahudumu wa baa hiyo waliandikiwa mashtaka ya kuwa wateja. Lakini faili ya marehemu haikufika mahakamani kujibiwa mashtaka. Bw Cheki Wairegi alishtakiwa kivyake kama muuzaji wa pombe kinyume na sheria,” yasema taarifa moja.

Bw Kinyua anasema kuwa huo ulikuwa uamuzi haramu wa kushtaki washukiwa hao kwa makosa yanayoonyesha kuwa yalikuwa ya kulazimisha.

Hicho ndicho kizungumkuti ambacho kwa sasa kinaendelea kuchunguzwa na vitengo kadhaa vya polisi na pia watetezi wa haki za kibinadamu, tayari hata maafisa waliokuwa kazini katika mkondo wa kisa hiki wakiwa tayari wameandikisha taarifa zao.

Marehemu amezikwa katika kijiji cha Gathigia-Irembu kaunti ndogo ya Maragua.