‘Tatizo la vijana kukosa kazi lastahili kushughulikiwa kwa ushirikiano’

‘Tatizo la vijana kukosa kazi lastahili kushughulikiwa kwa ushirikiano’

NA LAWRENCE ONGARO

UKOSEFU wa ajira ni changamoto kubwa ambayo tayari inaendelea kushuhudiwa hapa nchini Kenya.

Jambo hilo pia limeweza kushuhudiwa zaidi barani Afrika ambayo ina kiwango kikubwa cha watu wasio na ajira.

Kulingana na wataalam wa kiuchumi na maendeleo jambo hilo ni donda dungu ambalo haliwezi kutanzuliwa mara moja.

Wakati huo pia imebainika kuwa ukosefu wa ajira imeweza kusababisha ukosefu wa usalama  na pia kuvuruga makazi ya jamii nyingi hasa barani Afrika na kwingineko ulimwenguni.

Kaimu Afisa Mkuu Mtendaji wa Hazina ya Maendeleo ya Vijana (NDYF), Bw Benson Muthendi alisema vijana wengi wamejiunga na kubuni njia zao za kipekee za kuanza ajira za kibinafsi.

“Njia hiyo ndiyo ya kipekee ya kuwapa mwelekeo wa kujitegemea kiajira bila kutegemea serikali ama mashirika mengine kwa kutafuta kazi,” alifafanua afisa huyo.

Alisema iwapo vijana wengi watajituma kwa kuwa wabunifu bila shaka shida za kutafuta ajira itapungua na serikali itapata hafueni kwa kuinua uchumi wake.

Kulingana na uchunguzi uliyofanywa hivi majuzi, imebainika kuwa wakati wa uchaguzi mkuu vijana wengi walitumiwa vibaya kupitia viongozi kwa lengo la kuahidiwa fedha kidogo.

Ilidaiwa kuwa jambo hilo linatendeka kila mahali hata barani Afrika ambapo vijana wasio na ajira hupotoshwa ili kuzua fujo kwa manufaa ya watu wachache.

Bw Muthendi alisema serikali inastahili kujitolea mhanga kuona ya kwamba vijana wanapewa mwongozo ili waweze kujisimamia wenyewe.

Alisema hata ingawa wanafunzi wengi hukamilisha masomo yao kutoka vyuoni lakini bado wengi wao wanastahili kupata mwongozo dhabiti ili kujiendeleza wenyewe.

Profesa Renson Muchiri wa chuo kikuu cha KCA jijini Nairobi, alipendekeza kuwa vyuo vya kielimu vinastahili kushirikiana na kampuni na mashirika mbalimbali ili wanafunzi wanapokamilisha masomo yao waweze kupata nafasi za kazi katika sehemu hizo.

Tayari vyuo viwili vimeungana РKCA na chuo cha Nottingham cha nchini Uingereza Рili kuona ya kwamba vijana wanapewa mwongozo dhabiti wa  masuala ya ajira.

Alitoa wito kwa serikali mpya iliyochaguliwa majuzi kufanya hima kuona ya kwamba maslahi ya vijana yanaangaziwa haraka iwezekanavyo.

“Tunaelewa vijana wengi nchini hawana ajira na kwa hivyo wanastahili kupewa nafasi ili wajikimu kimaisha,” alieleza Prof Muchiri.

Tayari imebainika wazi kuwa vijana wengi wasio na ajira wamevunjika moyo na kukosa matumaini maishani.

Aliyasema hayo jijini Nairobi alipofanya kikao na washika dau wa kielimu na wanafunzi wa chuo cha KCA.

  • Tags

You can share this post!

Ziwa Naivasha hatarini

Kilichosukuma Ruto kuteua wanasiasa wengi mawaziri

T L