Habari Mseto

TAVETA: Wagonjwa wa saratani kupata afueni katika kituo kipya

November 12th, 2018 2 min read

Na LUCY MKANYIKA

KITUO cha kutoa matibabu kwa waathiriwa wa magonjwa sugu eneo la Pwani, Coast Hospice, kimefungua tawi jipya katika kaunti ya Taita Taveta ili kupambana na ongezeko la visa vya saratani.

Wadau wa afya katika eneo hilo wameripoti ongezeko la visa vya saratani ambao ni kati ya magonjwa yanayoongoza katika kusababisha vifo duniani.

Mkurugenzi wa kituo cha Coast Hospice tawi la Mombasa Dkt Eric Ochieng, alisema Kilifi inaongoza kwa visa hivyo ikizingatiwa kuwa asilimia 50 ya wagonjwa wanaopata huduma katika kituo cha Mombasa ni wenyeji wa kaunti hiyo.

“Taita Taveta inafuata kwa idadi ikifuatiwa na kaunti ya Mombasa,” akasema Dkt Ochieng.

Dkt Ochieng alisema kuwa kituo hicho kipya kilichoko katika hospitali ya Moi mjini Voi kinapania kupunguzia mzigo wagonjwa wa kaunti hiyo ambao hulazimika kusafiri hadi Mombasa ili kupata huduma.

Kituo hicho kinatarajiwa kuhudumia takriban wagonjwa 200 kila mwezi haswa wanaotoka vijijini.

Kando na saratani, wahudumu watahudumia wagonjwa wa msukumo wa damu, sukari, magonjwa ya moyo, figo, mapafu na mengineyo.

Mkurugenzi wa Ushauri katika shirika la Kenya Hospice Palliative Care Association (KEHPCA) Dkt Asaph Kinyanjui alisema kuwa jumla ya vituo 31 vimefunguliwa katika maeneo mbalimbali nchini.

“Tuna jumla ya wahudumu 70 ambao hutusaidia katika kufanikisha wajibu wetu wa kusaidia wagonjwa hawa ambao wengi wao wamekata tamaa maishani,” akasema.

Mmoja wa bodi hiyo Bw Faustine Mghendi alisema kuwa kituo hicho vilevile kitatoa mafunzo kwa wahudumu wa afya wa nyanjani ili kuhakikisha kuwa huduma zao zinafika mashinani.

Alisema ipo haja ya kuhamasisha umma juu ya lishe bora kwani huchangia pakubwa katika ongezeko la magonjwa haswa ule wa saratani.

“Vilevile tutakuwa tukiwatembelea wagonjwa walioko hospitalini na nyumbani na pia kutoa ushauri kwao na familia zao,”akasema.

Mbunge wa Voi Jones Mlolwa alisema bunge la kitaifa limekuwa likijadiliana kuhusu umuhimu wa kuongeza bajeti ya kupigana na saratani.

“Wakenya wamekuwa wakiumia sana na ni jambo la kusikitisha kuona kuwa baadhi yao hawana uwezo wa kugharamia matibabu yao,”akasema.

Aliwataka Wakenya kujisajili na hazina ya afya ya NHIF ambayo itaweza kugharamia matibabu ya saratani.

Vilevile Mwakilishi wa wanawake wa kaunti hiyo Bi Lydia Haika alisema ipo haja ya wadau wote kushirikiana ili kupiga na jana hilo.

“Hili ni janga la kitaifa na tunafaa tulikabili sote kwa pamoja,” akasema.

Naibu gavana wa Taita Taveta Bi Majala Mlaghui alisema serikali hiyo ina wajibu wa kuwapa wenyeji huduma bora za kimatibabu.

Bi Mlaghui alisema kuwa serikali imeipa idara ya Afya kipau mbele kwa kuhakikisha kuwa wanaboresha huduma za afya.

“Kutoa huduma kama hizi kwa wagonjwa wanaogua magonjwa sugu ni jambo la busara mno. Kama kaunti tutaunga mkono kituo hiki,” akasema.

Wagonjwa wa saratani katika eneo la Pwani hukimbilia hospital ya Coast General iliyoko mjini Mombasa ili kupata matibabu na hivyo kusababisha msongamano katika kituo hicho.