Makala

'Tawi' na 'jani' ni sehemu mbili bainifu katika mmea

May 22nd, 2019 2 min read

Na ENOCK NYARIKI

TUTAYAANGAZIA maneno mawili ya msingi mno.

Nimelitumia neno “msingi” kwa maana ya jambo ambalo watu hujipurukusha nalo kwa kudhani kuwa wanalifahamu.

Baadhi ya watu hulitumia neno ‘‘jani’’ wanaporejelea tawi. Utata katika kuyatofautisha maneno haya yamkini unatokana na kushikamana sana kwa sehemu hizo mbili za mmea.

Mwanafunzi mmoja wa darasa la pili alichora jani alipoulizwa kuchora tawi.

Mwalimu aliusahihisha mchoro huo wa jani hata ilipokuwa bayana kwamba mwanafunzi mwenyewe alikosea.

Jambo hilo lilionyesha bayana kwamba hata mwalimu mwenyewe hakujua tofauti baina ya tawi na jani licha ya kuwa ndiye aliyemwambia mwanafunzi kuchora.

Tukio jingine linalothibitisha kwamba maneno mawili tuliyoyataja huwakanganya watu lilitokea Jumapili iliyopita mhubiri fulani alipoyakosoa matumizi ya neno ‘tawi’ yanavyojitokeza katika Yohana 15.

Katika sura hii, Kristo anazungumzia kuhusu mzabibu wa kweli, matawi na mkulima.

Mhubiri mwenyewe alionelea kwamba badala ya tawi, neno jani lingetumiwa kwa maana iliyokusudiwa ingawa kusema kweli Kristo mwenyewe anataja dhana ‘tawi lisilozaa matunda’ – jambo linalolipa neno hilo maana stahiki.

Maelezo kwamba jani ni sehemu ya tawi yanaweza kuwa na upungufu kwa sababu mbili kuu.

Mashina

Kwanza, baadhi ya majani huunganishwa kwenye mashina ya mimea wala si matawi.

Pili, baadhi ya mimea huwa na majani wala si matawi. Mfano mzuri wa mimea hiyo ni mgomba ambao huwa na majani mapana ambayo huunganishwa kwao na sehemu fulani mfano wa kitawi.

Neno tawi linafafanuliwa kamusini kuwa ni sehemu ya mti inayoota majani, maua na matunda.

Katika utangulizi wa makala haya, tumesema kwamba tawi na jani ni sehemu mbili za mmea zinazoshikamana sana. Jambo hilo linajitokeza katika fasili hii ambapo neno jani limerejelewa.

Kwa hivyo, jani ni sehemu ya mmea yenye rangi ya kijani na umbo bapa inayoota kwenye shina au tawi la mti.

Kile kinachojitokeza katika fasili mbili za hapa juu ni maelezo mduara ambapo maneno mawili tuliyoyataja yanafafanuana.

Tutaje hapa kwamba dhana ‘umbo bapa’ hurejelea chochote chenye uso mpana na kina chembamba.

Ahasili, tawi ni ile sehemu ya mmea ambayo kwayo majani, maua na vikonyo vya matunda huota ilhali jani ni sehemu ya mmea yenye umbo pana na rangi ya kijani ambayo huota kwenye shina la mti au tawi la mmea.

Katika muktadha mwingine, neno tawi hutumiwa kurejelea sehemu au vitengo vya kitu fulani, kwa mfano, sehemu za mashirika au kampuni.