Michezo

Tebogo apewa Sh11 milioni na nyumba wananchi wakifurahia holidei Botswana

Na GEOFFREY ANENE August 9th, 2024 2 min read

CHIPUKIZI Letsile Tebogo amefanya raia wenzake wa Botswana wapate likizo ya nusu siku Ijumaa baada ya kushindia taifa hilo dhahabu ya kwanza kabisa tangu ianze kushiriki Michezo ya Olimpiki mwaka 1980.

Tebogo almaarufu Schoolboy, alishinda dhahabu ya kihistoria kwa katika mbio za mita 200 kwa sekunde 19.46 na kupongezwa na raia wa Botswana akiwemo Rais Mokgweetsi Eric Keabetswe Masisi aliwapa likizo hiyo washerehekee mafanikio hayo ya kihistoria.

Alibwaga Waamerika Kenneth Bednarek (19.62) na bingwa wa mbio za mita 100, Noah Lyles (19.70) ambaye alisalia kujikuna kichwa sakafuni baada ya kushindwa. Lyles alikuwa amepigiwa upatu kuibuka mshindi.

Kutokana na kuwa Tebogo amekuja Kenya mara kadhaa kushiriki mashindano ya Kip Keino Continental Tour, Wakenya wengi kwenye mitandao ya kijamii sasa wamemchangamkia wakidai ni wao pamoja na medali yake.

Mbali na umaarufu, Tebogo atapokea tuzo ya mshindi ya Sh6.4 milioni (Dola za Amerika 50,000) kutoka kwa Shirikisho la Riadha Duniani kwa ushinda wake.

Tebogo kifua mbele akielekea kushinda mbio hizo za 200m Ijumaa. PICHA | REUTERS

Nchini mwake, gazeti la Mmegi limeripoti kuwa kampuni ya Choppies Botswana itamtuza Sh9.5 milioni (Pula 1 milioni) na bidhaa za vyakula na matumizi ya nyumbani za Sh23,775 kwa mwaka mzima. Gazeti hilo maarufu linasema kuwa Tebogo pia atazawadiwa nyumba kutoka kwa serikali.

Vile vile, Baraza la kitaifa la michezo ya Botswana (BNSC) litampa Tebogo Sh2.3 milioni katika mpango wa kutuza wanamedali wa taifa hilo. Kwa kufuzu tu kushiriki Olimpiki, Tebogo pia alipokea Sh284,751.

Tebogo ni Mwafrika wa pili kupata medali katika mbio za mita 200 za wanaume kwenye Olimpiki baada ya Frankie Fredricks kutoka Namibia aliyenyakua nishani ya fedha mwaka 1992 mjini Barcelona nchini Uhispania na pia 1996 mjini Atlanta nchini Amerika.

Mtimkaji huyo mwenye umri wa miaka 21 anayeshikilia rekodi ya Afrika ya 19.50, alikimbia vizuri kutoka mwanzo kabla ya kuonyesha wapinzani wenzake kisogo baada ya kupiga kona.

Katika makala yaliyopita mjini Tokyo nchini Japan, Andre De Grasse kutoka Canada alishinda dhahabu akifuatiwa na Bednarek na Lyles katika usanjari huo.

Rekodi ya dunia ya umbali huo bado inashikiliwa na Usain Bolt kutoka Jamaica 19.19 tangu mwaka 2009. Bolt pia ni mshikilizi wa rekodi ya Olimpiki baada ya kufyatuka 19.30 mjini Beijing, Uchina mwaka 2008.