Teddy Mwambire achaguliwa Spika wa Bunge la Kaunti ya Kilifi

Teddy Mwambire achaguliwa Spika wa Bunge la Kaunti ya Kilifi

NA ALEX KALAMA

ALIYEKUWA Mbunge wa Ganze Teddy Mwambire amechaguliwa kuwa Spika wa Bunge la Kaunti ya Kilifi na kuchukua nafasi ya Jimmy Kahindi anayeondoka.

Bw Mwambire ambaye pia ni mwenyekiti wa chama cha ODM kaunti ya Kilifi amemshinda mshindani wake wa karibu James Mlewa baada ya kupata kura 37 dhidi ya kura 13 za Mlewa wakati wa duru ya kwanza ya upigaji kura.

Hata hivyo katika kinyang’anyiro cha kuwania nafasi ya Naibu Spika wa bunge hilo, kivumbi kikali kimeshuhudiwa baina ya wagombea wawili wa mrengo wa Azimio na ule wa Kenya Kwanza ambapo mrengo wa Azimio umeongozwa na Naftali Kombo wa chama cha Jubilee huku wa Kenya Kwanza ukiwakilishwa na Agnes Sidi wa chama cha ANC. Upigaji kura umefanyika kwa duru ya pili, kwa vile hakuna mgombea yeyote aliyepata thuluthi mbili ya kura zilizohitajika katika duru ya kwanza.

Kombo wa mrengo wa Azimio amepata kura 21 kwenye duru ya kwanza naye Sidi wa Kenya kwanza akipata kura 20 huku Thaura Mweni wa chama cha PAA akipata kura 9. Katika duru hiyo ya kwanza diwani mmoja aligoma kupiga kura. Mshindi alikuwa Bw Kombo katika duru ya pili.

Spika Mwambire aliapishwa mara moja baada ya kula kiapo cha afisi katika bunge, huku spika anayeondoka Kahindi akimpongeza rasmi na kumkabidhi zana za uongozi.

Awali, kulizuka taharuki kabla ya upigaji wa kura ambapo baadhi ya madiwani wanaoungwa mkono na Kenya Kwanza walipinga kufanyika kwa uchaguzi huo wakilalamika kwamba baadhi ya madiwani wa mrengo wa Azimio walikuwa wamekosa kuzingatia sheria za uchaguzi huku karani wa bunge hilo Micheal Ngala akikosa kuwachukulia hatua licha ya kudai kwamba baadhi yao walikuwa wakipiga picha karatasi za upigaji kura ambapo ni kinyume cha sheria.

  • Tags

You can share this post!

CHARLES WASONGA: Bei ya Sh3,500 ya mbolea si afueni tosha...

Mahakama yamfuta kazi kinara wa chama cha wazazi nchini

T L