Makala

TEKNOHAMA: App za kukusaidia kupunguza unene

March 3rd, 2020 2 min read

Na LEONARD ONYANGO

IDADI ya Wakenya walionenepa kupindukia inazidi kuongezeka humu nchini, kulingana na ripoti mbalimbali za hivi karibuni.

Ripoti iliyotelewa hivi karibuni na Shirika la Afya Duniani (WHO) kwa ushirikiano na Shirika la Watoto la Umoja wa Mataifa (Unicef) na Benki ya Dunia inaonyesha kuwa zaidi ya Wakenya milioni 3.4 ni wanene kupindukia.

Asilimia 4.1 ya watoto wa chini ya umri wa miaka mitano ni wanene kuliko kawaida na asilimia 13 ya vijana barobaro wa kati ya umri wa miaka 13 na 18 wana uzani wa juu zaidi kuliko wastani.

Ripoti iliyotolewa na Kituo cha Kuzuia Maradhi (CDC) ilisema kuwa wanawake wanakuwa wanene kwa kasi ikilinganishwa na wanaume humu nchini.

Ripoti hiyo ya CDC ilionyesha kuwa mwanamke mmoja kati ya watatu ni mnene kupindukia.

Utafiti uliofanywa mnamo 2018 nchini Kenya na Chuo Kikuu cha Göttingen cha nchini Ujerumani kwa ushirikiano na Taasisi ya Kimataifa ya Kutafiti Sera Kuhusu Vyakula (IFPRI) ilifichua kuwa ongezeko la watu wanene kupindukia linasababishwa na ulaji wa vyakula vinavyouzwa kwenye maduka makuu kwa wingi.

Watafiti hao walisema tatizo la watu wanene kupindukia limeongezeka maradufu ndani ya kipindi cha miaka 10 iliyopita.

Walisema idadi kubwa ya watu, haswa katika maeneo ya mijini, wanakula vyakula vinavyouzwa madukani badala ya kupika wenyewe nyumbani.

Unene kupindukia husababisha presha ya damu, kisukari, kiharusi, maradhi ya kibofu cha mkojo, mshtuko wa moyo, ugumu wa kupumua, matatizo ya akili, maumivu ya mwili kati ya magonjwa mengineyo.

Kulingana na kituo cha CDC, unene kupindukia husababishwa na ulaji wa vyakula kiholela bila kuzingatia kanuni za afya.

Lakini ikiwa wewe ni mwathiriwa wa unene kupindukia bado kuna matumaini ya kurejelea hali ya kawaida. Wataalamu wanashauri watu kufanya mazoezi mara kwa mara ili kupunguza uzito.

Mbali na mazoezi, mamia ya programu za simu (app) zimetengenezwa kusaidia watu kula lishe bora kwa kuzingatia kanuni za afya.

Baadhi ya app zinazosaidia watu kupunguza uzito ni Smart Diet, MyFitnessPal, Lose It, Edo, Yummly, FitYou na See How You Eat kati ya nyinginezo nyingi.

Wizara ya Afya ya nchini Uingereza inafanya majaribio kuhusu app ya Smart Diet ambayo inaaminiwa kuwa huenda ikasaidia watu kupunguza uzito.

App hiyo hushauri watu kula na kuepuka aina fulani ya vyakula. Kadhalika inahesabu hatua mtumiaji anapotembea au kukimbia.

MyFitnessPal hukushauri kuhusu athari za aina ya chakula unachotaka kula. Kwa mfano, ikiwa unataka kula nyama, app hii hukueleza kiwango cha mafuta ambayo huenda ukaongeza mwilini hivyo kukufanya kuwa mnene kupindukia.

App ya Lose It inakushauri kupunguza kiasi cha chakula unachotaka kula. Kabla ya kuanza kula unapiga picha sahani ya chakula na app hii hukushauri kupunguza au kuongeza.

Unapoenda katika duka kuu kununua vyakula app ya Edo inakushauri ni aina ipi ya chakula huenda ikakufanya kuwa mnene kupindukia.

Katika karatasi iliyofungiwa bidhaa katika duka kuu huwa kuna mistari inayofahamika kama barcode.

Mistari hiyo huwa na taarifa kuhusu bei ya bidhaa husika na vitu vilivyotumiwa kutengeneza bidhaa hiyo. App ya Edo husoma mistari hiyo na kukupa ushauri ikiwa inafaa kwa afya yako au la.

App ya Yummly hukusaidia kuandaa orodha ya vyakula unavyofaa kupika kila siku huku app ya FitYou ikikusaidia kujadiliana na marafiki kuhusu vyakula vinavyofaa kwa afya ili kupunguza uzito.

App ya See How You Eat inakushauri kukoma kula chakula kupindukia.