Makala

TEKNOHAMA: Hatua kubwa katika matibabu ya ubongo

September 17th, 2019 2 min read

Na LEONARD ONYANGO

JE, unaweza kumaliza siku ngapi bila kutumia simu yako ya mkononi?

Kulingana na tafiti zilizowahi kufanywa, watu wenye uraibu wa simu hukumbwa na msongo wa mawazo wanapokosa kutumia kifaa hicho kwa wastani wa masaa manne tu.

Hii ni kwa sababu kimekuwa sehemu ya maisha yao kiasi kwamba wengi huonekana wagonjwa simu inapoishiwa na chaji au kupotea.

Utafiti uliofanywa na shirika la kimataifa la kutafiti matumizi ya intaneti na simu la nchini Uingereza -YouGov, ulibaini kuwa idadi kubwa ya watu wamekuwa waraibu wa simu kiasi cha kulazimika kuangalia skrini za simu zao mara kadhaa wanapokuwa mezani na familia zao au marafiki.

Hii ni kwa sababu, mbali na mawasiliano, simu ina vitabu, michezo ya kompyuta, benki, na kadhalika.

Ripoti ya Mamlaka ya Mawasiliano nchini (CA) ya hivi karibuni inaonyesha kuwa kila Mkenya huzungumza kwa simu wastani wa dakika 80 kwa mwezi.

Ni kutokana na uraibu huo ambapo wanasayansi wamekuwa wakitafiti kwa lengo la kubaini athari za simu kwa afya ya watumiaji.

Utafiti uliofanywa hivi karibuni na Taasisi ya Kutafiti Miale ya Kielektroniki nchini Amerika (RSNA) unasema kuwa uraibu wa simu huathiri utendakazi wa ubongo.

Watafiti hao pia walisema kuwa idadi kubwa ya watu, haswa vijana, wanapoteza muda mwingi wakiangalia simu zao badala ya kutangamana na wenzao.

Utafiti wa kina wa kimataifa uliofanywa miaka michache iliyopita ulisema kuwa hawakupata ushahidi kwamba miale ya kielektroniki, maarufu Radiofrequency (RF), inayotolewa na simu inadhuru afya.

Lakini Shirika la Afya Duniani (WHO) mnamo 2011 liliwataka watumiaji kutotumia muda mwingi wakiwasiliana kwa simu kuepuka madhara ya miale ya RF.

Lakini sasa simu huenda ikawa muhimu katika matibabu ya ubongo.

Hii ni baada ya kikosi cha watafiti kutoka Amerika na Korea Kusini kubuni kifaa cha kielektroni kitakachopeleka dawa moja kwa moja kwenye ubongo.

Kifaa hicho kitaelekezwa na simu ya mkononi, maarufu smartphone.

Aidha kimeonyesha kufaulu baada ya kufanyiwa majaribio kwenye panya, kulingana na ripoti iliyochapishwa katika jarida la Nature Biomedical Engineering.

Kifaa hicho ambacho watafiti hao wamekipa jina la Wireless Optofluidic Brain Probes, kinapeleka dawa kwenye ubongo kulingana na maelekezo ya simu.

“Kifaa hicho kisichounganishwa kwa waya na simu huenda kikawa hatua kubwa katika kutoa matibabu ya ubongo,” akasema Raza Qazi, mmoja wa watafiti hao kutoka Taasisi ya Elimu ya Sayansi na Teknolojia nchini Korea Kusini.

Watafiti hao pia wanaamini kuwa huenda kikawasaidia madaktari kubaini maradhi ndani ya ubongo.

Baadhi ya magonjwa hayo ni maradhi ya kupoteza kumbukumbu, kiharusi, mzongo wa mawazo, kiharusi kati ya mengine.

Chafanyiwa majaribio

Kifaa hicho hakijaanza kutumiwa kwa binadamu na kingali kinafanyiwa majaribio zaidi katika panya.

Kulingana na Qazi, mbinu zinazotumiwa kwa sasa kupeleka dawa katika ubongo zinapoteza wakati na zinaweza kusababisha madhara kwa sababu vifaa vinavyotumika ni vigumu.

Kifaa kipya ni chepesi na chembamba sawa na unywele hivyo kinapenya kwenye ubongo kwa urahisi. “Kinatumia teknolojia ya ‘bluetooth’ kuwasiliana na simu,” anasema Qazi.

Watafiti hao wanasema teknolojia hiyo huenda ikatumiwa kubadilisha mienendo ya baadhi ya wanyama kwa kulenga baadhi ya maeneo katika bongo zao.

Prof. Michael Bruchas ambaye pia alishiriki katika utafiti huo anasema teknolojia hiyo itawezesha wataalamu wa matibabu kuvumbua dawa za kukabiliana na maumivu ya kichwa na matatizo mengineyo ya ubongo. “Tunangoja kwa hamu na ghamu kutumia kifaa hicho kipya kutafiti matibabu ya kukabiliana na maumivu ya kichwa, uraibu na matatizo mengineyo ya kiakili kama vile mzongo wa mawazo,” anasema Prof Bruchas.