Makala

TEKNOHAMA: Simu huenda ikatumiwa kupima UTI

January 28th, 2020 2 min read

Na LEONARD ONYANGO

MAAMBUKIZI ya mfumo wa mkojo (UTI) yamekuwa yakihusishwa na wanawake, lakini wataalamu wa afya wanasema kuwa wanaume wako hatarini pia.

Maambukizi hayo hutokea bakteria wanapojazana katika mrija (urethra) unaopitisha mkojo.

Mrija huo huanzia katika figo na kuendelea katika kibofu cha mkojo na kumalizia katika uke au uume.

Maambukizi ya UTI katika kibofu cha mkojo miongoni mwa wanaume ni adimu kwani wao wana mrija mrefu wa urethra kuliko wanawake.

Visa vingi vya maambukizi ya UTI miongoni mwa wanaume hutokea kwenye korodani (prostate).

Dalili za UTI miongoni mwa wanaume ni mkojo wenye harufu mbaya, mkojo unaoonekana kama vumbi, kuwa na matone ya damu kwenye mkojo kati ya nyinginezo.

Dalili za maambukizi hayo miongoni mwa wanawake ni haja ya kutaka kukoja mara kwa mara, maumivu kupitisha mkojo na maumivu katika sehemu ya chini ya tumbo.

Maambukizi ya UTI husababishwa na bakteria wanaojulikana kama Escherichia coli (E. coli).

Kufanya mapenzi kiholela bila kinga pia kunaweza kusababisha maambukizi ya UTI.

Kulingana na wataalamu wa kiafya, baadhi ya aina za mbinu za kupanga uzazi pia zinasababisha maambukizi ya UTI miongoni mwa wanawake.

Maradhi hayo ya UTI yanatibiwa hospitalini. Madaktari wanaonya kuwa kuchelewesha matibabu huenda kukasababisha figo kuharibika.

Wanawake wajawazito wanaochelewa kupata matibabu ya UTI wako katika hatari ya kujifungua mapema kabla ya kukamilisha wiki 40.

Kuchelewesha kwa matibabu hayo pia kunafanya mrija wa urethra kukonda.

Kulingana na Shirika la Afya Duniani (WHO), asilimia 50 ya wanawake hupatwa na maambukizi kabla ya kuzeeka.

Wanasayansi katika Chuo Kikuu cha Bath cha Uingereza wametengeneza teknolojia inayowezesha watu kutumia simu kupima maambukizi ya UTI.

Kulingana na watafiti hao, simu inakuwezesha kujua ikiwa una UTI au la ndani ya dakika 25.

Wanasema teknolojia hiyo huenda ikawa afueni kwa watu wanaokwepa kwenda hospitalini kupimwa kutokana na hofu kwamba huenda wakapatikana na maradhi ya zinaa.

“Simu inatoa kidokezo ikiwa mtu ana maambukizi ya UTI na kisha mwathiriwa anaweza kwenda hospitalini ithibitishwe,” unasema utafiti wa wataalamu hao.

Watafiti hao pia wanasema teknolojia hiyo inalenga kusaidia watu wanaoishi katika maeneo ya vijijini mbali na vituo vya afya. Hii ni kwa sababu teknolojia hii haihitaji umeme.

Watafiti hao wamechapisha uvumbuzi wao kwenye jarida la Biosensors and Bioelectronics.

Kamera ya simu hutumiwa kutambua bakteria wa E. coli kwenye sampuli ya mkojo. Bakteria hii husababisha asilimia 80 ya UTI, kulingana na WHO.

Sampuli ya mkojo huwekwa kwenye kipande cha plastiki ambacho humulikwa na kamera ya simu.

Kamera hubaini mabadiliko ya rangi ya sampuli ya mkojo na hata kupima msongamano wa bakteria wa E. coli.

“Vipimo hivi havihitaji ujuzi mwingi na pia teknolojia hii haihitaji kiasi kikubwa cha kawi,” wanasema watafiti hao.

Hata hivyo, teknolojia hiyo huenda ikawa na kibarua kigumu kuidhinishwa kwani taasisi za kusimamia matibabu katika mataifa mbalimbali duniani zimekuwa zikitilia shaka vipimo vya maradhi vinavyofanywa kwa simu.

Taasisi hizo zinasema kuwa kuwa iwapo zitaruhusu simu kutumika kupima maradhi, huenda zikafanya watu kutoenda hospitalini kupimwa maabarani.

Taasisi hizo pia zinasema kuwa vipimo vya simu huenda vikapotosha wagonjwa.

Wataalamu wanasema kuwa kunywa maji mengi huenda kukakusaidia kujiepusha na maambukizi ya UTI.

“Kunywa kiasi kikubwa cha maji humfanya mtu kukojoa mara kwa mara hivyo kutoa bakteria nje ya mfumo wa mkojo,” linasema shirika la WHO.

Aidha kudumisha usafi baada ya kwenda haja kubwa na ndogo husaidia.

Kojoa baada ya kushiriki mapenzi na kisha unywe maji angalau glasi moja. Kufanya hivyo, kutasaidia kutoa nje bakteria wanaosababisha UTI.

Epuka kutumia vipodozi ukeni.