Makala

TEKNOHAMA: Simu, TV hudumaza ubongo wa watoto wachanga – Utafiti

November 12th, 2019 2 min read

Na LEONARD ONYANGO

JE, watoto wako wa chini ya umri wa miaka mitano wanafanya nini nyumbani wakati huu ambapo shule zimefungwa?

Ikiwa wanatumia muda wao mwingi kuchezea simu au kutazama filamu katika televisheni, basi wako hatarini kwani huenda wakawa mbumbumbu darasani siku za usoni.

Wanasayansi sasa wanasema kuwa ubongo wa watoto wa chini ya umri wa miaka miwili wanaotumia muda mwingi wakitazama skrini ya simu, televisheni au kompyuta hufifia na wanashindwa kuzungumza vyema.

Watafiti hao wanasema watoto hao pia hulemewa katika somo la hisabati na hata kushindwa kukumbuka mambo wanayofundishwa darasani.

Watafiti katika Hospitali ya Cincinnati ya nchini Amerika walibaini kuwa ubongo wa mtoto anayechezea simu, kompyuta au kutazama runinga kwa muda mrefu hunyong’onyea.

“Huu ndio utafiti wa kwanza kuhusisha kutazama runinga au skrini ya simu kwa muda mrefu na athari zake kwa ubongo wa watoto wadogo wa chini ya miaka mitano,” akasema Dkt John Hutton, mmoja wa watafiti katika hospitali ya Watoto ya Cincinnati.

Matokeo ya utafiti huo yalichapishwa katika jarida la kitafiti la JAMA Pediatrics.

“Ubongo wa mtoto hukua kwa kasi ndani ya umri wa miaka mitano,” akasema Hutton. Tafiti ambazo zimewahi kufanywa hapo awali zimebaini kuwa watoto wanapotumia simu au kutazama runinga kwa muda mrefu, hushindwa kuwa makini darasani na hata kuwa na tabia mbovu.

Inaaminika kwamba watoto wanaochezea simu au kutazama runinga kwa muda mrefu wanachelewa kuzungumza, hulala usingizi wa mang’amung’amu na hukosa uhusiano wa karibu na wazazi wao.

Wanasayansi pia wamebaini kwamba wazazi wanaopendelea kucheza na simu au kutazama runinga kwa muda mrefu watoto wao pia huwa na tabia hiyo.

Wataalamu wanapendekeza kuwa watoto walio chini ya umri wa miaka mitano wachezee simu au watazame runinga kwa muda usiozidi saa moja kwa siku.

Watafiti wanaonya kuwa idadi ya watoto walio na ubongo hafifu huenda ikaongezeka duniani kwani watoto hutembea na simu wanapokuwa sebuleni au kitandani.

“Wanaweza kwenda na simu kitandani, wanaweza kuitumia wanapokula, wanapokuwa garini na hata uwanja wa michezo,” wanasema watafiti hao.

Wataalamu pia wanasema wazazi wanadhuru afya ya watoto wao kwa kuwapa simu wakiwa wangali wachanga zaidi kama vile mwaka mmoja.

“Asilimia 90 ya watoto wanatumia simu wakiwa na umri wa kuanzia mwaka mmoja,” anasema Hutton.

Mashine ya MRI

Watafiti hao walitumia mashine ya MRI, ambayo hutumiwa kunasa picha za sehemu za ndani mwilini, kuchunguza bongo za watoto.

Walipima bongo za watoto 47 (wavulana 20 na wasichana 27) ambao hawakuwa wameanza kwenda shule ya chekechea.

Kabla ya kufanyiwa vipimo vya MRI, watoto hao waliulizwa maswali ili kupima uelewa wao na kukumbuka mambo.

Wazazi wao pia walipewa fomu kujaza wakati ambao watoto wao wanatumia kutazama runinnga au simu wanapokuwa nyumbani au ndani ya gari.

Matokeo yalionyesha kuwa watoto waliotumia simu au kutazama runinga kwa zaidi muda wa saa moja unaopendekezwa, walikuwa na ubongo hafifu ambao haujakua vyema. Sehemu nyeupe ya ubongo wa watoto waliokuwa wakichezea simu kupita kiasi haikuwa imekua vyema na ilionekana kuwa na dosari.

Sehemu nyeupe ya ubongo ina idadi kubwa zaidi ya seli ambazo huelekeza mwili kuhusu kitu kinachostahili kufanywa.

Misuli iliyoko ndani ya ubongo inapokosa kukua vyema inasababisha mtoto kufikiria polepole.

Sehemu nyeupe ya ubongo ndiyo huhusika na mazungumzo na kumbukumbu.