Makala

TEKNOHAMA: Tumia app zilizokubalika pekee kwa afya yako

February 11th, 2020 2 min read

Na LEONARD ONGANGO

KATIKA mtandao wa Google Play Store, kuna maelfu ya programu za simu (apps) zinazodai kusaidia watu kuboresha afya zao kwa kuzingatia lishe, kukabiliana na msongo wa mawazo, kulala vyema, kupima presha, kati ya matatizo mengineyo ya kiafya.

Kwa mfano, kuna zaidi ya app 1,000 zinazodai kusaidia watu kujua namna ya kutambua ikiwa wana maradhi ya kansa na jinsi ya kuyazuia.

Kwa mfano, apu ya Cancer Risk Calculator inadai kuwa inasaidia watu kujua ikiwa wana kansa au la kwa kutathmini taarifa kuhusu vyakula unavyokula, ikiwa unavuta sigara au miongoni mwa vigezo vinginevyo.

Baadhi ya app hizi pia zinadai kutoa ushauri kuhusu jinsi ya kutibu kansa kwa kula vyakula vya kiasili.

Kadhalika, kuna maelfu zinazodai kutoa suluhisho kwa nguvu za kiume.

Kwa mfano, moja inadai vyakula kama vile pilipili au mayai vinasaidia kuongeza hamu ya mapenzi huku zingine zikidai kutoa ushauri kuhusu jinsi ya kupanga uzazi.

Wataalamu wanasema kutumia app kama njia ya kupanga uzazi si salama kwa asilimia 100.

Wanasema kuwa asilimia 20 ya wanawake wanaotumia kwa uaminifu app ya simu kama njia ya kupanga uzazi hujipata na ujauzito.

Madaktari pia wanaonya kuwa japo baadhi zinasaidia, zingine zinapotosha.

Watu wanafaa kutumia app zinazohusiana na hospitali au taasisi tajika za afya.

Miongoni mwa zinazoaminika ni WHO HTS Info ambayo inamilikiwa na Shirika la Afya Duniani (WHO). App hiyo hutoa taarifa kuhusu maambukizi ya virusi vya HIV na magonjwa ya zinaa.

Shirika la WHO pia linamiliki app ya WHO Info ambayo hutoa taarifa kuhusu afya kote duniani.

Nchini Kenya, app ya Medbit iliyotengenezwa na Richard Okenye inawezesha wagonjwa kuwasiliana na madaktari moja kwa moja, jijini Nairobi.

App hiyo inasaidia kupunguza msongamano hospitalini kwani wagonjwa wanaweza kuafikiana na madaktari muda wanaofaa kukutana nao.

Soko la app za matibabu halijadhibitiwa hivyo kutoa mwanya kwa walaghai kutengeneza zinazopotosha wagonjwa.

Tafiti ambazo zimewahi kufanywa zinaonyesha kuwa nyingi hazijafanyiwa majaribio ya kisayansi kuthibitisha ufaafu wazo.

Ili kuepuka kupotoshwa, bunge la Ujerumani wiki iliyopita lilipitisha sheria inayowaruhusu madaktari kuwashauri wagonjwa kuhusu zile sahihi wanazofaa kutumia.

Waziri wa Afya wa Ujerumani Jens Spahn, alisema kuwa nchi hiyo ni ya kwanza kutunga sheria kuhusu matumizi ya app. Miongoni mwa app ambazo madaktari watashauri wagonjwa wao kutumia ni zile zinazosaidia kukabiliana na ugonjwa wa kisukari, matibabu ya msongo wa mawazo na presha ya damu.

Taasisi ya Kudhibiti Matumizi ya Dawa na Vifaa vya Matibabu (BfArM) itatathmini ubora kwa kuzingatia vigezo kama vile utunzaji wa siri za wagonjwa, urahisi wa kutumiwa kabla ya kuidhinisha madaktari kushauri wagonjwa kuzitumia.

Watengenezaji sharti washawishi taasisi ya BfArM kuwa app zao zinasaidia kuboresha afya.

Taasisi ya Matibabu ya Uingereza (NHS) na ile ya Amerika (FDA) tayari zimependekeza baadhi ambazo zimefanyiwa majaribio na wataalamu wa afya.

Kabla ya kupakua app kutoka mtandaoni, soma tathmini (reviews) ambazo zimeandikwa na watu wengine ambao wamewahi kuitumia.

Iwapo watumiaji hao wanaisifu, basi app hiyo huenda inafaa. Iwapo tathmini ni hasi, haifai achana nayo.

Kadhalika, chunguza kampuni inayomiliki app hiyo. Ikiwa imetengenezwa na taasisi, kampuni au shirika la kuaminika, kama vile FDA, NHS, WHO au wizara ya Afya ya Kenya, na kadhalika, inafaa.

App zinazokuhimiza kula lishe bora zinafaa lakini zile zinazodai kutoa tiba ya maradhi hazifai kuaminiwa na badala yake muone daktari.