Makala

TEKNOHAMA: Twitter kuwalinda waathiriwa wa kifafa

December 31st, 2019 2 min read

Na LEONARD ONYANGO

MTANDAO wa kijamii wa Twitter umepiga marufuku picha za kuchezacheza na kubadili rangi maarufu APNG kwa lengo la kuwalinda watu wenye kifafa dhidi ya kukumbwa na mshtuko wa ubongo na kupoteza fahamu.

Mtandao wa Twitter ambao unamilikiwa na kampuni ya Facebook, ulichukua hatua hiyo baada ya wadukuzi kutumia teknolojia kuondoa vikwazo vilivyokuwa vimewekwa na mtandao huo wa kijamii.

Wadukuzi hao walitumia picha hizo katika kaunti ya Twitter ya shirika la huduma kwa watu wenye kifafa nchini Amerika, Epilepsy Foundation.

Kulingana na Twitter, picha hizo zinazochezacheza na kumetameta kwa kasi bila kikomo zinaweza kusisimua ubongo wa watu wenye kifafa na kuwafanya kuanguka na kupoteza fahamu.

Mtandao wa Twitter, Jumanne ulisema kuwa uligundua kwamba baadhi ya wadukuzi waliwezesha watumiaji wa Twitter kupakia picha hizo ambazo ni hatari kwa waathiriwa wa kifafa.

“Tunataka kila mmoja kuwa salama katika mtandao wa Twitter,” ukasema mtandao wa Twitter.

“Picha za APNG zilikuwa zinaleta raha mtandaoni, lakini tumegundua kuwa wakora wamedukua mtandao na sasa watu wanazipakia kiholela. Tumeamua kuzipiga marufuku. Hii ni kwa ajili ya watu ambao hudhurika wakitazama picha zinazochezacheza kwa kasi, wakiwemo watu wenye kifafa,” ukaongezea.

Wadukuzi hao walidukua akaunti ya shirika la Epilepsy Foundation mnamo Novemba ambao ni mwezi wa kuhamasisha watu kuhusu maradhi ya kifafa nchini Amerika.

Shirika la Epilepsy Foundation linasema kuwa tayari limeshtaki mmiliki wa akaunti ya Twitter iliyotumiwa katika udukuzi huo.

Wataalamu wanasema kuwa video fupi ambazo huchezacheza kwa kasi huku zikitoa mwangaza wa rangi mbalimbali zinadhuru ubongo, haswa wagonjwa wa kifafa.

Kwa mujibu wa mtandao wa epilepsy.com unaomilikiwa na shirika la Epilepsy Foundation, asilimia 3 ya waathiriwa wanaweza kupoteza fahamu kutokana na mwangaza unaochezacheza kama ule unaopatikana katika kumbi za burudani. Hali hii ya waathiriwa kupoteza fahamu kwa muda kwa sababu ya mwangaza inafahamika kama photosensitive epilepsy.

Watoto wachanga na vijana wa chini ya umri wa miaka 20 ndio huathiriwa zaidi na mwangaza.

Mwangaza unaoweza kusababisha waathiriwa wa kifafa kupoteza fahamu ni maandishi yanayopita kwa kasi katika runinga, baadhi ya michezo ya kompyuta, na kadhalika.

Waathiriwa wa kifaa wanafaa kuepuka kutazama mwangaza unaochezacheza kama ule unaopatikana katika majumba ya burudani na maandishi yanayopita kwa kasi kwenye runinga.

Mbali na mwangaza, mambo mengine yanayoweza kusababisha waathiriwa wa kifafa kupoteza fahamu ghafla ni kutotumia dawa waliyopewa na daktari, msongo wa mawazo, matumizi ya mihadarati, hedhi, kutokula na kuwa na maradhi yanayopandisha joto la mwili.

Ili kuepuka kupoteza fahamu, waathiriwa wa kifafa wanashauriwa kutumia dawa mara kwa mara, kulala vyema, kujaribu kuepuka msongo wa mawazo, kujiepusha na ubugiaji wa pombe na kula vizuri.

Je, unaweza kufanya nini mwathiriwa wa kifafa akipoteza fahamu na kuanguka ghafla?

Wataalamu wanashauri kwamba watu waliokaribu na mwathiriwa waondoe vitu vigumu ili asiumie. Usijaribu kumshika ili asijigeuze. Hakikisha kuwa anapata hewa ya kutosha na usijaribu kuziba mdomo wake.

Madai kwamba mwathiriwa wa kifafa anaweza kumeza ulimi wake anapoanguka ni dhana potofu, kwa mujibu wa wataalamu wa afya.

Imani nyingine potofu zinazohusiana na kifafa ni kwamba waathiriwa huwa wamerogwa, wamelaaniwa, familia zao zina mizozo au wanaweza kuwaambukiza watu wengine.

Kadhalika, hakikisha kwamba mwathiriwa haingii ndani ya maji.

Kifafa ni hali ya ubongo kupoteza fahamu na kumfanya mwathiriwa kuanguka chini huku akitokwa na povu mdomoni.

Kulingana na Shirika la Kushughulikia Masilahi ya Waathiriwa wa Kifafa nchini Kenya (Kawe), asilimia 80 ya watu wanaougua wanaweza kutibiwa iwapo hali hiyo itagunduliwa mapema.