Makala

Teknolojia inayofanya kazi kama ubongo wa binadamu huenda ikatumika kutengeneza chanjo dhidi ya Corona

March 7th, 2020 2 min read

Na MARY WANGARI

SHIRIKA moja la Amerika kwa jina DeepMind limefichua kuhusu kazi yake ya ziada inayohusu teknolojia inayofanya kazi kama ubongo wa binadamu – Artificial Intelligence (AI) – inayochanganua kwa kina muundo wa protini sita zinazohusishwa na virusi vya Corona vya Wuhan, maarufu kama SARS-CoV-2 au kitu kinachosababisha COVID-19.

Mradi huo mpya wa elimu kimitambo unatumai matokeo yanaweza kuwasaidia wanasayansi kuunda chanjo inayoweza kuzuia na kukomesha kusambaa kwa virusi vya Corona duniani.

Kwa kufahamu muundo wa protini wa virusi hivyo, wanasayansi wanaweza kuelewa jinsi virusi hivyo vinavyofanya kazi na jinsi vinavyoweza kukomeshwa.

Baadhi ya maabara zimesambaza data yao binafsi kuhusu protini iliyozalishwa kikompyuta au kiutafiti na sasa shirika la DeepMind limejitosa katika ulingo huo likiwa limepania katika juhudi zake za AI.

Wakosoaji wanaweza kuona hatua hii kama njama za kupigia debe ilhali matokeo yapo ikiwa unataka kuyaopoa na kuyajaribu.

Kando na hilo, sababu nzuri ya kutumia maarifa kimitambo ni kwamba yanatoa matokeo haraka kushinda kazi ya maabara na yaliyosahihi zaidi.

“Tunasisitiza kwamba bashiri hizi za muundo hazijathibitishwa kiutafiti lakini tunatumai zitachangia katika udadisi wa jamii ya wanasayansi kuhusu jinsi virusi hivyo vinavyofanya kazi; na kutumika kama tasnia ya kuzalisha majaribio kwa kazi za utafiti siku za usoni ili kuunda tiba,” lilisema mnamo Alhamisi.

Wasomi hao walitumia AlphaFold, mfumo uliozinduliwa mwishoni mwa 2018, kutabiri miundo sita mikuu ya protini kwa SARS-CoV-2.

Walitumia data kutoka kwa Raslimali ya Protini Ulimwenguni, datakanzi wazi inayofafanua aina na kazi ya maelfu ya protini zilizotolewa kutoka miradi ya kuainisha vitengo, ili kusaidia AlphaFold katika tabiri zake.

Datakanzi hiyo, kutokana na thamani yake, hutumia mtindo unaofahamika kama “uundaji wazi” kubashiri miundo ya protini ya virusi hatari vya Corona.

Haijabainika bashiri hizo sita ni sahihi kiasi gani maadamu ni machache mno yanayofahamika kuhusu ndwele hiyo.

Muundo mmojawapo hata hivyo unafanana na mmoja ulioundwa na kundi la wanasayansi katika Chuo Kikuu cha Texas, Austin na Taasisi ya Kitaifa ya Uzio na Maradhi ya Maambukizi, shirika lililo chini ya Taasisi ya Afya Nchini Amerika.