Makala

TEKNOLOJIA: Wanafunzi wako tayari, nani atawafundisha usimbaji wa programu?

September 24th, 2019 5 min read

NA FAUSTINE NGILA

NI Jumatano mchana katika mji wa Meru, ambapo Taifa Leo Dijitali imetembelea Shule ya Msingi ya St Paul iliyoko mita chache kutoka katikati ya mji wa Meru. 

Wanafunzi kadhaa wamekusanyika darasani huku wakiongeleshana kwa sauti za chini na wengine wakiingia kuketi. Taswira ya nyuso zao na jinsi wanavyotembea kwa mwendo wa asteaste zinadhihirisha fika ujasiri na umakini wao.

Katika kona moja ya darasa hili ni wasichana walioonekana kuzama katika simu zao kwa mapenzi na tabasamu kana kwamba wamesheherekea siku yao ya kuzaliwa jana.

Katikati kuna marijali ambao wanashiriki katika mdahalo kwa kunong’onezeana, wengine wakivitingisa vichwa na wengine wakigongesha mikono yao kwenye madawati kusisitiza maoni yao.

Ghafla mwanamume wa miaka 25 anaingia darasani na kusimama tisti mbele ya darasa, kisha kujitambulisha kama Bw Alex Guantai, mratibu wa mradi wa Code Mashinani katika shule za msingi na upili mwaka eneo la Meru.

Mratibu wa mradi wa Code Mashinani katika shule za msingi na upili mwaka eneo la Meru Bw Alex Guantai akielezea wanafunzi manufaa ya teknolojia. Picha/ Faustine Ngila

WARSHA

Warsha ya teknolojia ya siku tatu imeandaliwa na wazazi wametakiwa kuwashirikisha wana wao wa umri wa miaka 6 hadi 18 kwenye warsha itakayotoa mafunzo ya teknolojia, ili kukuza viongozi wa baadaye.

“Tumepanga kambi ya kufunza kodi ili kuwasaidia wanafunzi kuimarisha fikra zao kufuatia changamoto katika mazingira wanamoishi na jinsi uvumbuzi wa kiteknolojia unaweza kuleta suluhu, ” anasema Bw Guantai.

Brian Mutuma, mwanafunzi wa kidato cha nne katika Shule ya Upili ya Mang’u anapania kuwa wakili atakapofuzu chuoni. Kulingana naye, ni wakati mwafaka kwa watu kuwa na uzoefu wa mabadiliko yanayochangiwa na teknolojia mpya.

“Teknolojia inasambaa kwa haraka na watu watakuwa wakiitegemea . Hii ni kwa sababu mtu hawezi kuwa hodari asilimia 100 ila utumiaji wa teknolojia utarahisisha mambo hata katika kazi tunazofanya,” anasema Brian.

Aidha anapinga madai kuwa teknolojia itawafanya wafanyikazi kutowajibika kwani itakuwa na manufaa zaidi.

“Watu lazima wajifunze kuikumbatia teknolojia na kuachana na hofu kuwa itawabandua na kuchukua nafasi asilia zote. Wanafaa kuona manufaa yake, ” anasema.

Anafunguka kuwa iwapo atapewa fursa, ataanzisha mtandao wa kijamii ambao utapunguza utumiaji wa karatasi hasa katika sekta ya uanasheria. Kulingana naye, visa vya kesi kutoendelea kutokana na ukosefu wa ushahidi vinaweza kusuluhishwa na teknolojia.

Hata hivyo Edwin Ikaria kutoka Shule ya Upili ya Thura anasema kuwa teknolojia imeleta madhara mengi.

“Napenda teknolojia ila imeleta madhara, wezi wanatumia mitandao kuiba, wanadukua benki na mitandao ya kijamii ,” analalamika Edwin.

Hata hivyo alishikilia kwamba ili kuinasua serikali kwenye mazimwi ya ufisadi, ni lazima teknolojia itumike.

TEKNOLOJIA KUZIMA UFISADI

“Mie huchukia visa vya ufisadi vinavyotendeka nchini. Naamini ipo siku uvumbuzi wa teknolojia itakayotambua wafisadi itaundwa ili kutatua tatizo hili,” anatoa matumaini Edwin.

Aliongeza kuwa mahakama zinachukua miaka na mikaka kukamilisha kesi zilizopo, jambo ambalo linafaa kusitishwa. Alitoa mifano ya waathiriwa wa dhuluma ambao hawawezi kupokea matibabu hospitalini kwa sababu ya kukosa fomu ya P3 ambayo kulingana naye, huchukuwa mda mrefu kutolewa.

Akiwa na miaka 18, Edwin anahofia ukosefu wa ajira kutokana na kuwepo kwa roboti. Hata hivyo,  Elizabeth Wanjiru, mwanafunzi wa darasa la nane katika Shule ya St Paul Academy ana maoni tofauti na na Edwin.

“Mimi na ithamini teknolojia kwa sababu inaboresha maisha kwani hizo roboti haziwezi kufanya kazi bila kudhibitiwa na mwanadamu, watu wanafaa kujifunza jinsi ya kuzimudu tu, ” anasema Elizabeth.

Anasisitiza kuanzishwa kwa jukwaaa la kuwasaidia wanafunzi ambao wazazi wao wanashindwa kulipa karo.

“Licha ya kukosa fedha za karo, ni haki kwa kila mtoto kupata elimu bora. Wazazi wenye mapato ya chini wanafaa kusaidiwa.”

Elizabeth anapania kuwa mwigizaji na angependa kuanzisha teknolojia ya kuboresha vipaji kama hivyo pamoja na kuhakikisha kuwa wanapata malipo kwa wakati.

Katoka Shule ya Upili ya Wasichana ya Kaaga, Jasmine Nkatha, mwanafunzi wa Kidato cha Kwanza analenga kuwa mtangazaji na angependa kutangaza taarifa za runinga siku moja ila kulingana naye, jambo hilo haliwezi kutimia hadi teknolojia iweze kuboreshwa.

Wanafunzi washiriki katika warsha ya teknolojia katika Shule ya Msingi ya St Paul’s mjini Meru. Picha/ Faustine Ngila

5G

“Ukitazama teknolojia ya hologram na video za 5G katika mtandao wa YouTube na kufikiria jinsi taarifa za siku za usoni zitakavyokuwa, utatambua kwamba kweli changamoto zipo.

“Nataka kuwa na uzoefu wa teknolojia na kuwasaidia watu hasa kule mashinani kupata taarifa za runinga,” anasema Nkatha.

Kulingana naye, ili kuepuka madhara ya teknolojia, ni lazima watu waifahamu teknolojia .

“Tumesikia madaktari wa upasuaji wakitumia roboti kuimarisha uhakiki katika operesheni zao, ila wao wamejifunza teknolojia hiyo kwanza,” anasimulia.

Jesse Nkatha, mwenye umri wa miaka 10 katika Shule ya Msingi ya St Paul’s Academy  anataka kuwa mchezaji bomba na mtajika wa kandanda, sio tu humu nchini bali hadi kimataifa.

“Napenda jinsi Messi alivyowalambisha sakafu wapinzani na kufuma mabao, najua ana bidii na baadhi ya makocha hutumia uchanganuzi wa data ili kumuongoza, ” alisema Jesse.

Pia anafahamu kuwa teknolojia zinazohusishwa na kandanda kama Video Assisted Referee (VAR) na ile ya kutambua mpira ukipita laini ya goli zinaleta usawa katika sekta hiyo. “Sipendi kuona timu ikishinda kwa kupendelewa,” anamalizia Jesse.

UZEMBE WA SERIKALI

Licha ya kuwepo kwa wanafunzi ambao wapo tayari kuisoma teknolojia, serikali na sekta binafsi zimezembea katika uanzilishi wa programu za usimbaji (coding) shuleni ili kuwasaidia wanafunzi.

Katika mataala mpya wa elimu , teknolojia ambayo ni nguzo kuu katika kuimarisha uchumi miaka inayokuja, imeachwa nje licha ya wanafunzi kuwa na ujuzi na hamu yake.

Bw Jesse Muchai ambaye ndiye afisa mkuu mtendaji na mwanzilishi wa Code Mashinani alisema kuwa ameweka mikakati ya warsha ya mafunzo ili kuwasaidia wanafunzi kuwa na fikra bora na bunifu.

“Wanadamu hawawezi kusoma vizuri hasa wakiwa na dharba. Tumewekeza kwa watoto kwa sababu wao wanafikiria umuhimu na manufaa na pia hupenda kujaribu vitu vipya na huamini wanachofunzwa bila kubisha, ”alisema Bw Muchai katika mahojiana na Taifa Leo Dijitali.

Licha ya juhudi zake, Bw Muchai anadai kuwa bado kuna mengi ya kufanywa ili kutimiza malengo hayo.

“Malengo yetu ni kuchochea wanafunzi wajiulize maswali muhimu kwani hata kuunda programu lazima uwe na elimu ya teknolojia,”  aliiongeza Bw Muchai.

Bi Peris Waithera, mwasisi mwenza wa Code Mashinani alisema ni njia bora ya kuwaelimisha wasichana kuthamini teknolojia na kuhakikisha kuna usawa wa 1:1 katika mafunzo yote. Hata, wanawake wanaonekana kuachwa nyuma.

“Wanawake wanaogopa teknolojia, wanahofia kujifunza sayansi, tekmolojia, hesabu na uhandisi. Tunataka kuto aiyo hofu na kuwaelewesha umuhimu wa teknolojia pamoja na kutatua chanagamoto wanazopata kama ukeketaji,” alisema Bi Waithera.

Baada ya ziara yetu maswali mawili ynaibuka: Je, ni nani atawafunza wanafunzi ujuzi huu iwapo taifa hili linalenga kujiandaa kwa mageuzi ya kiteknolojia? Nani atawafunza jinsi ya kusimba (code) programu na tovuti zitakazoleta suluhu?

Watoto kutoka China hufunzwa jinsi ya kusimba kuanzia wakiwa miaka mitano ili kuwawapa uzoefu katika ulingo wa teknolojia mapema.

Austria, Bulgaria, Denmark, Estonia, Ufaransa, Hungary, Ireland, Lithuania, Malta, Uhispania, Poland, Ureno, Finland, Slovakia na Uingereza pia zimeanzisha mfumo huo wa usimbaji katika shule za msingi na upili.

Kennedy Kanyi, mwenye miaka 27, mwanaprogramu ambaye alianzisha lugha ya usimbaji ya BraceScript mwaka wa 2017, ni mfano bora wa vipaji vilivyomo humu nchini.

Miradi kama African Girls Can Code Initiative ambao unafanywa kuanzia mwaka wa 2018 hadi 2022 ni hatua mwafaka ila serikali za Afrika zinafaa kufunza na kukuza vipaji vya kusimba katika shule za umma.

Bitange Ndemo, profesa wa masuala ya biashara katika Chuo Kikuu cha Nairobi anasema kwamba miradi kama ya Code Mashinani ni mizuri na serikali inafaa kuwafunza wanafunzi kusimba kuanzia umri mdogo.

“Tunafaa kuanza kuwasaidia watoto kusoma na kutatua shida zilizopo wangali wachanga. Wanafunzi wa chekechea wanafaa kuzoeshwa kutumia programu ambazo zitawapanua akili,” anasema Prof Ndemo.

Shule ya Montessori ndiyo anayoamini kuwa mfano bora katika kutekeleza mtaala mpya wa elimu unaowatayarisha wanaafunzi kuwa viongozi wa baadaye na kukabili mawimbi ya kiteknolojia yanayokuja.

“Mfumo unaowafanya wanafunzi kujibu maswali kwa kuchagua jibu sahihi hautosaidia kamwe.Serikali inafaa kuiga mfumo unaotumika katika shule ya Montessori katika mtaala mpya wa elimu na pia kuufanya nafuu kwa wazazi,” anaeleza Prof Ndemo.

 

Imetafsiriwa na Fatuma Bugu