Makala

TEKNOLOJIA: Watoto wa Mombasa wanavyounda programu za kompyuta

September 3rd, 2018 2 min read

DIANA MUTHEU NA PETER MBURU

KWA Paul Akwabi, inawezekana kwa watoto wachanga kuanzia miaka tisa hivi kufunzwa masuala ya ubunifu ili kuboresha bongo zao na kuwainua kielimu na kimaisha.

Hili ni jambo alilopata kujua wakati aliposafiri ng’ambo na kupatana na watoto wachanga ambao ujuzi wao wa kiteknolojia ulimshangaza.

“Nilitaka kujua ni vipi mtoto mchanga hivyo huko Uropa alielewa teknolojia vyema hata kunishinda nikiwa mtu mzima. Nilifahamu kuwa watoto katika maeneo ya Uropa, India na Amerika wana vikundi vya kujifahamisha kielimu na teknolojia,” asema Bw Akwabi.

Akwabi alifurahishwa na namna watoto walitilia maanani umuhimu wa kusoma kwa kutumia teknolojia na hivyo akaanza utafiti kubaini baadhi ya mambo waliyofunzwa wanafunzi.

Lakini alishangaa kutambua kuwa watoto walikuwa na ufahamu mkubwa namna za kuunda mambo bunifu ya kiteknolojia ya kusaidia kurahisisha kufanya jambo Fulani (softwares), huku wakirahisisha miundo yao kuwafaa katika shughuli mahususi wanazofanya.

Alijipa changamoto kuwa walichokuwa wakifanya watoto wa kizungu ni jambo ambalo pia watoto wa kiafrika wanaweza kufunzwa na kuboreshewa maisha yao kwa kuongezewa ubunifu.

Ni hivyo, Bw Akwabi alivyoanzisha kikundi cha Tech Kids Africa ambayo sasa yeye ni mkurugenzi. Kupitia klabu hiyo iliyopewa jina ‘Swahilipot’, anatoa mafunzo ya kibinafsi ambapo anawafunza watoto kuhusu dhana tofauti za teknolojia.

Kwa sasa klabu hiyo ina zaidi ya watoto 50 wa kati ya miaka tisa na 17, japo alipoanzisha mwaka uliopita alikuwa na watoto watano pekee na kipakatalishi kimoja cha kutolea mafunzo.

“Kupitia mafunzo haya tulibaini kuwa ni rahisi kwa watoto kuja na mawazo mapya bunifu na kuyawasilisha,” akasema.

Mnamo Machi mwaka huu, aliandaa maonyesho kwa watoto hao kuonyesha weledi wao kwenye masuala ya teknolojia, ambapo walijizolea zawadi kochokocho ili wazidi kutumia teknolojia kwa njia zinazofaa.

Na hatua za Bw Akwabi kuwapa watoto ubunifu wa kiteknolojia haijakosa kutambuliwa kwani kampuni ya Global Ventures ambayo huhimiza matumizi ya njia bunifu kusuluhisha matatizo ya jamii iliichagua klabu hiyo kati ya kumi katika Africa.

“Tuliorodheshwa nambari tatu Afrika kuwa kikundi ambacho kinatoa mafunzo ya umuhimu na busara kwenye sekta ya elimu,” akasema.

Klabu hiyo aidha ilishiriki shindano la ‘Make it Africa’ ambapo kati ya washiriki 600 iliorodheshwa kuwa kati ya 30 bora.

Juni mwaka huu, Bw Akwabi alisafiri kuelekea Ujerumani baada ya Tech Kidz Africa kuorodheshwa tano bora, kati ya vikundi vinavyokuza ubunifu katika shindano jingine la dunia.

Kupitia juhudi zake, watoto wengi wameweza kutengeneza apu zinazoweza kusuluhisha matatizo hasa kwenye sekta za mawasiliano, usalama na burudani nchini.

“Mmoja wa wanafunzi wangu wa miaka 12 alitengenezea kampuni moja ya kuuza magari apu na kampuni hiyo ikamlipa,” akasema Bw Akwabi.

Maombi yake sasa ni kwa serikali kutambua juhudi zao na kuwapa msaada unaofaa, ili wafikie watoto zaidi.

“Tunapanga kufanya makongamano na nchi zingine ili kubadilishana mawazo. Huu ni wakati mwema kwa taifa letu kutupa mkono hasa kwa kupata vifaa kwani ni bei ghali,” akasema mtaalam huyo.

Alisema klabu hiyo inapania kushirikiana na wa vikundi vingine na kutafuta watu wa kuwapa msaada, ili kuwawezesha watoto hao kudhihirishia ulimwengu ubunifu wao.

“Pia ninapanga kuunda academia ya kutoa mafunzo ya teknolojia kwa watoto wa kati ya miaka saba na 17, ili kukuza vizazi vijavyo kuwa na ubunifu wa kutosha kusuluhisha baadhi ya matatizo ambayo tunakumbana nayo kama taifa,” akasema.

Bw Akwabi alisomea taaluma ya Teknolojia ya Mawasiliano (IT) kwatika chuo kikuu cha Technical University of Mombasa (TUM) kuanzia 2011.