Kimataifa

Teknolojia ya 5G kutetemesha mitandao 2019

January 14th, 2019 1 min read

MASHIRIKA Na PETER MBURU

Kampuni zaidi zimekuwa zikishirikiana na kubadilishana mawazo kuhusu namna ya kuwezesha dunia kutumia intaneti ya 5G.

Wakati wa kongamano la kidunia kuhusu teknolojia lililoandaliwa Jijini Las Vegas, Marekani wiki iliyopita, kampuni mbalimbali zilionyesha namna intaneti hiyo ambayo itakuwa na kasi ajabu itainua utendakazi wa mitandao.

Ikianza kazi, intaneti ya 5G itawezesha watumizi wa mitandao kufanya mambo mbalimbali kwa kasi, takriban mara 10 zaidi ya ile ya 4G. baadhi ya huduma ambazo zitanufaika na intaneti hiyo ni kama kuingia katika tovuti, ku’daonlodi’ nyimbo ama filamu ama kutazama filamu moja kwa moja mitandaoni.

Teknolojia hiyo inatarajiwa kuanza kufanya kazi US kuanzia 2020, japo baadhi ya kampuni zimeeleza kuwa zinalenga kuanza kuitumia mwaka huu.

Kampuni ya Verizon ilisema kuwa intaneti hiyo ya 5G itasaidia hata katika sekta ya afya na madaktari wa upasuaji kurahisisha kazi ili kufikia habari muhimu za mazoezi hayo kwa haraka.

“5G ni ahadi ya mengi mazuri zaidi kuliko yale yote tumeshuhudia katika teknolojia,” Afisa Mkuu Mtendaji wa kampuni hiyo Hans Vestberg akasema.

Kampuni hiyo imeunda mtambo ambao unageuza signali za intaneti ya 5G kuwa Wi-fi katika nyumba za wateja wake. Lakini bado haijatengeneza intaneti itakayotumiwa na bidhaa za kutembea nazo kama simu ama tarakilishi.

Afisa Mkuu Mtendaji wa kampuni ya Samsung HS Kim alisema kuwa intaneti ya 5G itaunganishwa na teknolojia ya AI, ambapo kwa pamoja teknolojia hizo zinaweza kuunganishwa kwa gari.

Kampuni zaidi zilizidi kuonyesha namna teknolojia ya 5G inakuja kufaa dunia, katika wakati huu ambapo utumizi wa mitandao umezidi kupanuka duniani.