Habari za Kitaifa

Wito Wakenya wakumbatie teknolojia ya AI kukabiliana na changamoto za kimaisha

February 23rd, 2024 1 min read

JOSEPH OPENDA Na KENNEDY KIMANTHI

KONGAMANO Kuu la nne la Nation kuhusu masuala ya kidijitali limekamilika kwa wito kwa Wakenya kujiandaa kwa matumizi ya teknolojia ya Akili Unde (AI) katika nyanja zote za maisha.

Wajumbe walikubaliana kwamba watu binafsi na taasisi zinahitaji kujifunza na kuzoea teknolojia mpya bila kujali taaluma zao.

Mnamo Ijumaa, wataalamu walibadilishana maono kuhusu taathira za AI katika kukabiliana na changamoto za ulimwengu nyakati hizi.

Haja ya ukumbatiaji wa maadili katika matumizi ya teknolojia hii ilitambuliwa huku washiriki wakihimizwa kuendelea kupanua ufahamu wao kuihusu katika soko la ajira na nyanja nyingine za ujuzi.

“Mafunzo ya kila mara ni muhimu sawa na uwekezaji katika utafiti. Hulka ya ubunifu ina manufaa makubwa katika enzi hizi za kidijitali na inatujuzu kuona namna ya kutumia AI kuimarisha utendakazi wetu,” akasema Mhariri wa NMG anayesimamia masuala ya Kidijitali Oliver Mathenge.

Kongamano hilo la siku tatu lililoandaliwa mjini Naivasha, Kaunti ya Nakuru liliwaleta pamoja viongozi, wadau katika sekta hii na wakereketwa wa teknolojia ya habari na mawasiliano (ICT).

Wajumbe walijadili athari za matumizi ya teknolojia ya AI katika sekta mbalimbali, kuanzia vyombo vya habari, afya na fedha.