Michezo

Ten Hag aungwa mkono licha ya matokeo duni ya Man U


UONGOZI wa klabu ya Manchester United umemuunga mkono kocha Erik Ten Hag huku wakisisitiza kwamba Mholanzi huyo ana uwezo wa kubadilisha timu hiyo inayoendelea kusuasua kwenye Ligi Kuu ya Uingereza (EPL).

Baada ya kumaliza katika nafasi ya nane msimu uliopita na kutwaa taji la FA Cup baada ya kushinda Manchester City 2-1, United wameanza msimu huu wa 2024/2025 vibaya, matokeo ambayo yamemweka kocha huyo kwenye presha kubwa kutoka kwa mashabiki wanaotaka atimuliwe.

Manchester United wanaokamata nafasi ya 14 jedwalini walianza kampeni ya EPL kwa ushindi wa 1-0 dhidi ya Fulham kabla ya kuchapwa 2-1 na Brighton na baadaye 3-0 na Liverpool ugani Old Trafford, Jumapili, Septemba 1, 2024.

Iwapo watashindwa na Southamptom mnamo Septemba 14, 2024, yatakuwa matokeo yao mabaya zaidi tangu msimu wa 1986/1987, walipookota pointi moja kutokana na mechi nne za kwanza, matokeo ambayo yalichangia kufutwa kazi kwa kocha Ron Atkinson, mikoba yake ikipewa Sir Alex Ferguson.

Kwa sasa angalau, Ten Hag anaungwa mkono katika mpangilio mpya unaoungwa mkono na mmiliki mwenza wa klabu hiyo, Sir Jim Ratcliffe.

Wakizungumza na waandsihi wa habari za michezo kabla ya kucheza na Liverpool, Jumapili, Septemba 1, 2024 Afisa Mkuu wa klabu hiyo, Omar Berrada na Mkurugenzi wa Michezo, Dan Ashworth walisema ingawa hakuna aliyehusika katika mjadala wa kuamua Ten Hag aendelee kuwa kocha mkuu kabla ya msimu kuanza, lakini walisisitiza kumuuunga mkono.

“Uamuzi ulitolewa kabla ya sisi kuwasili, lakini tuauunga mkono uamuzi huo. Tumekuwa naye hata wakati wa msimu wa kununua wachezaji na tutaendelea kufanya kazi pamoja,” alisema Berrada.

“Jukumu langu ni kumuunga mkono kwa vovyote vile, katika masuala yote na kumpa nafasi ya kunoa wachezaji na kumsaidia katika kutekeleza mbinu zake za kiufundi ipasavyo, lengo likiwa kusaidia timu ipate ufanisi.

“Kazi yetu sio kuondoa wachezaji klabuni, bali hatuwezi kuwazuia kuondoka wanapotaka kuhama. Awe Jadon, Scott (McTiminay) au Aron (Wan-Bissaka). Tuna wachezaji wengi wazuri ambao tunaamini wana uwezo wa kujaza nafasi zao vyema.”