Habari Mseto

Tenda za serikali sasa kushindaniwa na wananchi

June 21st, 2018 1 min read

Na BERNARDINE MUTANU

Serikali imeanzisha mpango wa kuweka wazi tenda zake kwa wananchi.

Mpango huo utaweka wazi kandarasi zote na mikataba iliyotiwa sahihi na serikali. Hiyo itawezekana kupitia kwa wavuti maalum, alisema Waziri wa Fedha Bw Henry Rotich Jumanne.

Alisema hatua hiyo imechukuliwa wakati ambapo serikali ina miradi mingi ya muundo msingi, ambayo inatarajia kutekeleza kwa kushirikiana na sekta ya kibinafsi.

Habari zitazowekwa katika tovuti hiyo ni kuhusiana na utambulisho, utaratibu wa kutayarisha na uagizaji wa huduma na bidhaa, utiaji sahihi wa kandarasi, ujenzi na uzinduzi wa miradi hiyo.

Kwa sasa kuna miradi zaidi ya 70 ambayo inatekelezwa kwa ushirikiano kati ya serikali, umma na sekta ya kibinafsi(PPP).

Alisema hatua hiyo ni ya kuimarisha uwazi katika operesheni za serikali. Baadhi ya miradi ni kama ujenzi wa barabara na bandari.