Michezo

Teranga Lions, timu pekee iliyosalia kuokoa Afrika Urusi

June 19th, 2018 2 min read

Na CECIL ODONGO

JE,  mbona mataifa yanayowakilisha Bara Afrika katika Kombe la Dunia mwaka huu yanasuasua ama ni kutokana na kiwango duni cha soka ya bara hili?

Katika Kidumbwedumbwe  cha mwaka huu bara la Afrika linaonekana litakosa  kupiga hatua iwapo matokeo ya mechi za makundi zilizosakatwa awali zitatiliwa manani.

Ni aibu ilioje kwamba Nigeria, Misri, Tunisia, Morocco hazijaweza kusajili ushindi wala sare yoyote mwaka huu japo mamilioni mwa mashabiki barani waliziwekea matumaini kuwika kwenye fainali za mwaka huu.

Nigeria maarufu kiama ‘Super Eagles’ waliowekewa nafasi kubwa kati ya timu hizo kutamba walishindwa kuifunga Croatia katika mechi yao ya kwanza ya Kombe la Dunia.

Licha kujivunia huduma za mastaa kama Obi Mikel, Victor Moses na Alex Iwobi, mibabe hao wa soka ya Afrika walikubali kichapo cha 2-0 mikoni mwa Croatia.

Timu hiyo kutoka Magharibi mwa Afrika ina mlima wa kuukwea katika kundi lao na itapiga hatua tu iwapo itaishinda Argentina na Jamuhuri ya Ice land ambao ni wapinzani wao waliosalia.

Kwa upande wao Misri walionyesha mchezo uliokwenda skuli japo kwa bahati mbaya walipokezwa kichapo katika dakika za lala salama na wapinzani wao Uruguay.

‘The Pharaohs’ wanatasakata leo dhidi ya wenyeji Urusi kati mchuano ambao lazima waushinde ili wawe katika nafasi nzuri ya kufuzu iwapo watawapiga Saudi Arabia ambao wanaonekana kama wanyonge kundini.

Kufuzu kwa timu hiyo kutategemea matokeo ya leo na iwapo watakubali kichapo,  hawatakuwa na jingine ila kuabiri ndege moja kwa moja hadi Cairo.

Morocco nao waliitia bara hili aibu ya mwaka kwa kukubali kulishwa  zana za mgoli na limbukeni mbumbumbu katika ulimwengu wa soka Iran. Hapana shaka kwamba nchi hiyo kutoka  kaskakazini mwa Afrika haina uwezo wa kuzifunga Ureno na Uhispania kulingana na jinsi ilivyocheza. Tegemeo la pekee walilobaki nalo ni bahati nasibu.

Kati ya timu wakilishi wa bara, Tunisia pekee ndiyo timu ya kuonewa fahari baada ya kufunga bao la kwanza la Bara dhidi ya Uingereza. Ingawa walilishwa kichapo cha 2-1 na Uingereza vijana hao walipigana kufa kupona katika mechi hiyo.

 Iwapo watapiku Ubelgiji na washinde wanyonge Panama itabakia kitendawili kitakachoteguliwa tu baada ya mtanange.

Tegemeo pekee lililosalia kwa mataifa ya Afrika ni ‘The lions of Teranga’ Senegal ambao wanatarajiwa kuyabeba masaibu ya bara zima watakapochuana na Poland inayojivunia mshambulizi matata Robert Lewandosky baadaye Jumanne.