Makala

TERESIA NJOKI: Ubunifu ni muhimu katika uigizaji

November 11th, 2020 2 min read

Na JOHN KIMWERE 

ANAHIMIZA wenzie wawe wabunifu katika sekta ya usanii pia wajitume kwenye gemu ili kukomesha kasumba ya kuketi kijiwe kusubiria ajira. Anasema ukuaji wa teknolojia duniani unatoa nafasi nzuri kwa wenye talanta kubuni ajira badala ya kusubiria kuajiriwa. 

Aidha anawashauri wasiwe wepesi wa kuvunjika moyo hasa matarajio yao yanapokwenda mrama. Hata hivyo anasisitiza kuwa  ‘mtaka cha mvunguni sharti ainame’ maana hakuna mafanikio hupatikana rahisi.

Haya ni maneno yake Teresia Njoki Kiratu ambaye kisanaa anafahamika kama Triza ama Tii anayejivunia kushiriki filamu nyingi tu ndani ya miaka mitatu iliyopita.

VIDEO VIXEN

”Nimepania kujituma mithili ya mchwa kudhihirishia ulimwengu kuwa Wakenya pia tunaweza kufanya vizuri katika tasnia ya uigizaji,” alisema na kuongeza kuwa anafahamu wengi wanamlinganisha na kioo cha jamii ambapo wana dada wenzie wanamtazama kwa makini wakipania kufuata nyayo zake.

Kando na kuwa mwigizaji kisura huyu pia ni video vixen na mwana mtindo anayesema kuwa masuala ya maigizo yalimvutia baada ya kutazama filamu iitwayo ‘Best Friends Forever’ ambapo Brenda Wairimu aliigiza kama mhusika mkuu.

”Kusema kweli mwigizaji huyo hunitia motisha zaidi katika masuala ya maigizo hasa kwa jinsi hufanya miondoko yake na bila shaka nimejifunza mengi kutokana na uigizaji wake”, akasema.

BABAYAO SERIES

Chipukizi huyu anajivunia kushiriki filamu kadhaa akiwa mhusika mkuu tangia aanze kujituma katika masuala ya maigizo. Kwa jumla ameshiriki filamu kama: ‘Eliminate Series’ (K24), ‘Tale of Kunta’, ‘Marriage in Kenya,’ ‘Babayao Series,’ Kina series (Maisha Magic plus), ‘ ‘Lover Girl (K24),’ na ‘Njoro wa UBA (Maisha Magic) kati ya zingine.

Katika mpango mzima kipusa huyu anasema analenga kuibuka mwigizaji mahiri duniani na kutinga upeo wa wasanii shupavu kama Angelina Jolie mzawa wa Marekani. Jolie anajivunia kushiriki  filamu nyingi tu ikiwamo ‘Wanted,’ ‘Maleficent,’ ‘Mr and Mrs Smith,’ ‘Original,’  na ‘Girl Interrupted.’

”Wana dada wenzangu wanastahili kufahamu kwamba uigizaji ni ajira kama nyingine ambapo hawana budi kujituma bila kulegeza kamba. Pili wanapaswa kujiheshimu nyakati zote pia wanapopata nafasi hawana budi kufanya kazi kwa kujitolea kadiri ya uwezo wao,” akasema.

YOGA

Binti huyu mwenye tabasamu ya kuvutia anasema anatamani sana kuwa miongoni mwa wasanii wanaokuza wengine ambapo analenga kuanzisha brandi yake ndani ya miaka mitano ijayo. Wakati wa mapumziko anapenda sana kushiriki tizi ya kunyoosha misuli kama yoga kati ya zingine.