Michezo

Terror Squad yajeruhiwa na KNH

December 11th, 2019 1 min read

Na JOHN KIMWERE

TIMU ya Terror Squad ilichomwa mabao mabaoi 2-1 na timu ya Hospitali ya Kitaifa ya Kenyatta (KNH) kwenye mechi ya Kundi B Ligi ya Taifa Daraja ya Pili iliyopigiwa Camp Toyoyo Jericho, Nairobi.

KNH ilitia kapuni pointi tatu na kutua mbili bora katika jedwali la kipute hicho. Nao wapigagozi wa PCEA Kikuyu walilipua Zetech University Kitivo cha Nyahururu mabao 4-2 huku Maafande wa Spitfire ilitoka sare ya mabao 2-2 dhidi ya Muchatha United.

Mchezo wa KNH na Terror Squad ulishuhudia msisimko mkali hata hivyo Collins Ochieng aliibuka shujaa alipotingia washindi mabao hayo.

”Nashukuru wenzangu kwa jinsi walivyojituma kukabili wapinzani wetu na kuwazidi maarifa,” nahodha wa KNH, Ben Obiri alisema.

”Vijana wangu wanahitaji kukuza buti kwenye juhudi za kupigania tiketi ya kupanda ngazi msimu ujao,” alisema kocha wa KNH na kuongeza kuwa wamepangwa kundi la kifo.”

KNH ilivuna ufanisi huo wiki moja baada ya kudhalilisha Kirigiti Community kwa mabao 5-1. Nazo timu za Maafande wa Waterworks na Kahawa United kila moja ilisajili mabao 2-0 dhidi ya Mwiki United na Thika Allstars mtawalia.

Waterworks iliyoshiriki kipute hicho kwa mara ya kwanza ilipata ufanisi huo kupitia Mogire Enock na Zuberi Mohamed waliotikisa wavu mara moja kila mmoja.

Katika jedwali la ngarambe hiyo, PCEA Kikuyu inaongoza kwa kufikisha pointi 17, mbili mbele ya KHN sawa na Spitfire tofauti ikiwa idadi ya mabao.