Tetemeko laua watu 1,000 Afghanistan

Tetemeko laua watu 1,000 Afghanistan

NA AFP

SHARAN, AFGHANISTAN

IDADI ya watu waliokufa kutokana na tetemeko la ardhi lililotokea nchini Afghanistan Jumanne imepanda hadi kufikia 1,000 huku wengine 1,500 wakijeruhiwa, kulingana na Idara ya Habari ya Serikali ya Taliban.

Jana, waokoaji walikuwa wakiendelea kuwasaka manusura katika mikoa ya Paktika na Khost iliyoathirika zaidi na tetemeko hilo la uzito wa 5.9 katika vipimo vya richer.

Tayari wakazi wa maeneo hayo wanakabiliwa na changamoto kubwa ya ukosefu wa mahitaji ya kimsingi tangu Taliban walipotwaa mamlaka nchini Afghanistan mnamo Agosti 2021.

“Watu wanachimba kaburi moja baada ya jingine ili kuzika wapendwa wao,” akasema Mohammad Amin Huzaifa, ambaye ni mkuu wa Idara ya Habari na Utamaduni katika utawala huo wa Taliban.

“Watu wangali wamekwama ndani ya vifusi,” akawaambia wanahabari.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN) Antonio Guterres alisema afisi yake imetuma wahudumu wa afya, dawa, vifaa vya matibabu, chakula na mahema katika eneo la mkasa.

Mnamo Jumatano jioni kiongozi wa Afghanistan, Hibatullah Akhundzada alielezea hofu kwamba idadi ya waliokufa huenda ikipita 1,000, shughuli za kusaka manusura zinapoendelea.

Tayari shughuli hizo zinaathiriwa na mvua kubwa inayoshuhudiwa maeneo hayo ya milima na kusababisha maporomoko ya ardhi.

“Lilikuwa tukio baya zaidi,” akasema Arup Khan, 22, anayeendelea kupata afueni katika hospitali moja katika mji mkuu wa mkoa wa Paktika, Sharan.

“Vilio vilitanda kila mahali. Watu na familia yangu kwa ujumla walifunikwa na matope,” akaongeza. Mkurugenzi wa Hospitali ya Sharan Mohammad Yahya Wiar alisema wanafanya kila wawezalo kuwatibu majeruhi wote.

“Nchi yetu ni masikini na inakosa rasilimali,” akaambia shirika la habari la AFP.

“Mkasa huu umesababisha changamoto kubwa ya kibinadamu. Ni sawa na kimbunga cha tsunami.”

Picha na video zilizochapichwa katika mitandao ya kijamii zilionyesha idadi kubwa ya nyumba zilizoharibika katika maeneo ya mashambani.

Mshirikishi wa shughuli za usambazaji za misaada ya kibinadamu nchini Afghanistan, Ramiz Alakbarov, aliwaambia wanahabari kwamba zaidi ya nyumba 2,000 ziliharibiwa katika tetemeko hilo.

WAFU WAZIKWA

Kanda za video zilizotolewa na utawala wa Taliban zilionyesha watu katika kijiji kimoja wakichimba mtaro mrefu kuzika wafu.

Kulingana na kanuni za Kiislamu, sharti wafu walazwe makaburini wakitazama Mecca.

Mkasa huo ni changamoto kubwa kwa utawala wa Taliban ambao umechangia nchini hiyo kutengwa na mataifa ya ulimwengu kutokana na itikadi zao za Kiislamu zinazowadhalilisha wanawake na wasichana.

Hata kabla ya Taliban kutwaa utawala wa Afghanistan, mashirika ya kukabiliana na mikasa haikuwa na uwezo na rasilimali za kupambana na majanga ya kimaumbile ambayo hukumba taifa hilo kila mara.

Mnamo Januari 2022 tetemeko mbili za ardhi ziliathiri mkoa wa Badghis ulioko magharibi mwa nchini hiyo.

Mnamo 2015, zaidi ya watu 380 waliuawa nchini Afghanistan na taifa jirani la Pakistan kufuatia tetemeko la ardhi lenye nguvu ya kima cha 7.5.

  • Tags

You can share this post!

WANDERI KAMAU: Mataifa ya Afrika yaungane kupata ufanisi wa...

MAWAIDHA YA KIISLAMU: Siku 10 za mwanzo za mwezi muhimu wa...

T L